Samia ataka Mwanza wakae mkao wa kula, SGR kufungua fursa kwao

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:25 PM Oct 08 2025
Samia ataka Mwanza wakae mkao wa kula, SGR kufungua fursa kwao.

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuufungua kiuchumi Mkoa wa Mwanza, kupitia Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Mwanza-Isaka, mkoani humo kujengwa vituo vitano vitakavyokuza uchumi huko.

Ameahidi hilo leo Oktoba 8, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Nyamagana mkoani humo ambapo maelfu ya wananchi wamejitokeza kumsikiliza mgombea huyo.

“Kipande  cha Mwanza-Isaka km 314 kinachojengwa kwa Sh. triloni tatu, kimefikia asilimia 63  kutakuwa na vituo vitano. Katika vituo hivyo kutajengwa maduka,  hoteli, nyumba za wageni, na serikali itajenga maghala ya kuifadhi bidhaa za kwenda nje ya nchi au Dar es Salaam. Hii ni fursa Mwanza kaeni mkao wa kula.

“Mradi wote ukikamilika Dar es Salaam- Mwanza ni saa nane tu.Gharama za kusafirisha bidhaa itashuka.Hiki ni kipimo cha kupunguza mfumuko wa bei na umaskini kwa kuwa watu wote watanunua bidhaa,” amesema.