Serikali kuboresha TEWW kuruhusu wengi kupata fursa

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 02:09 PM Aug 28 2025
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda
Picha: Mtandao
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ameahidi kuiboresha zaidi Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ili kuhakikisha wananchi wengi walio nje ya mfumo rasmi wa elimu wanapata fursa ya kujifunza na kuongeza ujuzi.

Prof. Mkenda alitoa ahadi hiyo jana katika kilele cha Maadhimisho ya miaka 50 ya TEWW yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisisitiza kuwa serikali imejipanga kuimarisha mfumo wa elimu ya watu wazima na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma kwa kukosa elimu.

“Tunajivunia hatua mbalimbali na Taasisi hii. Leo tunasherehekea miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na tunaona matokeo chanya kwa sasa asilimia 83 ya Watanzania wanajua kusoma, kuhesabu na kuandika,” alisema Prof. Mkenda.

Alisema serikali itaendelea kusambaza miundombinu ya elimu nchi nzima ili kuhakikisha kila mkoa unakua na kampasi ya vyuo vikuu, shule za msingi na sekondari ili kufanikisha upatikanaji wa elimu kwa wote.

Katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Prof. Philipo Sanga, aliwasilisha mapendekezo manne ya kuboresha taasisi hiyo.

Mapendekezo hayo ni pamoja na kuandaa waraka maalumu kwa wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari wakashindwa kuendelea ili waweze kupata elimu nje ya mfumo rasmi.

Kila kata kuwa na kituo jumuishi cha ujifunzaji jamii kwa ajili ya mafunzo mbalimbali yatakayosaidia kuongeza wigo wa elimu na ujuzi wa wananchi.

Kurekebisha miongozo ya kamati kuanzia ngazi ya kituo hadi taifa ili iendane na mahitaji ya sasa kutokana na baadhi ya wajumbe waliokuwa kwenye kamati za awali kutoendelea kushiriki.

Kuunda Idara Maalum ya Elimu ya Watu Wazima kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa ili kuongeza ufanisi na usimamizi wa programu za elimu kwa watu wazima.

Prof. Sanga aliongeza kuwa utekelezaji wa maazimio hayo utawezesha taasisi hiyo kuongeza ubunifu na kuhakikisha elimu inawafikia watu wengi zaidi, hususan waliokosa nafasi kwenye mfumo wa kawaida wa elimu.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia elimu, Atupele Mwambene, alisema TEWW imechangia kwa kiwango kikubwa kupunguza ujinga nchini na kuwasaidia wananchi kupata maarifa kushughulikia changamoto zao za kiuchumi na kijamii.

Atupele alisema, utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo ni sehemu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia Sera ya Elimu ya Elimu ya mwaka 2014, toleo la 2023 ambayo inalenga kujenga mfumo wa elimu bila ukomo kwa kila Mtanzania.