Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeendesha Kongamano la 15 la Afya ya Kinywa na Meno likilenga kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa afya ya kinywa na meno, sambamba na kutoa mapendekezo ya kisera kwa Serikali ili kuboresha huduma hizo nchini.
Kongamano hilo limewakutanisha wataalamu wa afya ya kinywa na meno, watafiti, watunga sera na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kujadili changamoto zinazokabili wananchi na namna ya kuzitatua.
Akifungua kongamano hilo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe, alisema Serikali imewekeza zaidi ya Sh bilioni 17 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kwa ajili ya kununua mitambo na vifaa vya kisasa vya huduma za meno katika hospitali zote nchini.
“Afya ya kinywa ni sehemu muhimu ya ustawi wa mwili mzima. Tunapaswa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kupiga mswaki mara mbili kwa siku, kupunguza ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi, na kutembelea madaktari wa meno mara kwa mara,” alisema Dk. Shekalaghe.
Aidha, alilisifu chuo hicho kwa ushiriki wake katika Utafiti wa Kitaifa wa Afya ya Kinywa na matumizi ya teknolojia za kidijitali katika sekta ya afya, akihimiza mashirikiano endelevu kati ya sekta binafsi, taasisi za elimu na serikali ili kufanikisha huduma bora za afya kwa wote.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya, alisema kongamano hilo ni sehemu ya juhudi za chuo hicho kuhakikisha elimu ya afya ya kinywa inakuwa endelevu na inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
“Tunapitia mitaala yetu ili iendane na mabadiliko ya teknolojia. Tunataka kizazi kipya cha wataalamu wa meno wawe na ujuzi wa kidijitali na wawe tayari kuhudumia jamii kwa ubunifu na weledi,” alisema Prof. Balandya.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya, Dk. Baraka Nzobo, alisema utafiti umeonyesha zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanakabiliwa na matatizo ya meno na fizi, huku watoto na watu wazima wakiongozwa na changamoto za kuoza meno, mpangilio usio sahihi wa meno na ugonjwa wa fizi.
Aliongeza kuwa uhaba wa wataalamu bado ni changamoto kubwa, kwani nchi inahitaji zaidi ya madaktari bingwa 300 wa meno, lakini waliopo hawazidi 100.
Kongamano hilo limeibua mjadala mpana kuhusu jukumu la jamii katika kulinda afya ya kinywa, likisisitiza kuwa elimu, tabia bora za kiafya na huduma zenye upatikanaji rahisi ni nguzo muhimu katika kujenga taifa lenye watu wenye afya bora na tabasamu endelevu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED