Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF), kupitia mradi wa CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa kwa ushirikiano na Wizara ya Nishati, umekabidhi rasmi kifaa cha kupima hewa chafu kwenye majiko ya kupikia.
Makabidhiano haya ni sehemu ya Utekelezaji wa Mradi wa CookFund unaolenga kuharakisha usambazaji wa nishati safi ya kupikia nchini.
Mashine hiyo, ambayo imekabidhiwa kwa kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) itasaidia kuimarisha uwezo wa shirika kupima na kuchambua kwa usahihi moshi mchafu unaotoka kwenye teknolojia safi za kupikia.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio, alisisitiza: “Hii ni hatua kubwa katika kuendeleza harakati za kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia nchini. Kifaa hiki kitatumika kupima aina ya gesi au moshi mchafu unaotokana na matumizi ya majiko yanayotengenzwa au kuingizwa hapa nchini. Kitasaidia kuthibitisha ubora wa vifaa vya kupikia, kupunguza gharama za upimaji na kusaidia wabunifu kuongeza uzalishaji.”
Serikali imekuwa ikihamasisha ajenda ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia na mkakati wa mawasiliano, ambazo zote zinalenga kuhakikisha asilimia 80 ya kaya zinazotumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
“Umoja wa Ulaya unajivunia kuwa sehemu ya jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania. Tutaendelea kuunga mkono juhudi hizi kama tunavyofanya kupitia Mradi wa CookFund na programu nyingine zinazofanana na hizo. Tunatarajia kifaa hiki kitawanufaisha zaidi wabunifu na wazalishaji—hasa kwa kupunguza gharama za upimaji. Hii itachochea ubunifu na kuongeza kazi ya utengenezaji majiko na kuharakisha upimaji na usanifishaji wa vifaa vya kupikia safi” amesema Marc Stalsmans, Mkuu wa Ushirikiano, EU Tanzania
Mradi wa CookFund, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya na kutekelezwa na UNCDF kwa niaba ya Wizara ya Nishati, umetoa ruzuku kwa wafanyabiashara wa kati (SMEs) na kuboresha uwezo wa mashirika mbalimbali kama njia ya kusaidia usambazaji wa teknolojia za kupikia safi sokoni.
Hadi sasa mradi umetoa ruzuku kwa biashara 78, kusaidia shule 41 kuanza matumizi ya Nishati safi ya kupikia, kunufaisha zaidi ya watu milioni 1.7, kutengeneza zaidi ya ajira 11,600.
Shigeki Komatsubara, Mwakilishi wa UNCDF Tanzania, amesema: “Tunaamini kuwa kifaa hiki kitatoa takwimu muhimu za kutathmini athari halisi za majiko ambayo hayajakidhi viwango ambayo yanaweza kuwa na athari kwa watumiaji na kuharibu mazingira.”
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Ashura Katunzi amsema: “Kupatikana kwa kifaa cha upimaji nchini ni hatua muhimu katika kupunguza gharama, jambo litakalosaidia kusogea karibu zaidi na usanifishaji wa vifaa vya kupikia safi. Tunaomba msaada zaidi ili tuweze kupanua huduma hizi kwenye mikoa mingine kama Dodoma, Mbeya na Mwanza”.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED