Tatizo akamatwa tuhuma za kumuua mama wa kambo kwa mapanga

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 05:51 PM Oct 07 2025
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Benjamin Kuzaga.

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linamshikilia Tatizo Mzumbwe, mkazi wa Kijiji cha Mapinduzi, Kata ya Masoko, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, kwa tuhuma za kumuua mama yake wa kambo kwa kumcharanga kwa mapanga kichwani kufuatia mgogoro wa mashamba.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Benjamin Kuzaga, amesema kuwa marehemu ni mwanamke mwenye ualbino aitwaye Marry Yohana (61).

Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, tukio hilo lilitokea Oktoba 6, saa 2:00 usiku, ambapo mtuhumiwa alimvamia mama yake wa kambo akiwa nyumbani na kumjeruhi kwa mapanga kichwani kabla ya kukimbia na kujificha.

“Baada ya tukio, askari wetu walianza msako mkali na kufanikiwa kumnasa mtuhumiwa akiwa amejificha katika eneo la Masoko,” amesema Kamanda Kuzaga.

Ameeleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa ardhi, ambapo kijana huyo alidai kutaka agawiwe mashamba ya baba yake kwa lengo la kuyauza.

“Tunachunguza zaidi mazingira ya tukio hili. Vijana wanapaswa kuacha tamaa ya mali na badala yake wafanye kazi kwa bidii kupata riziki halali,” ameongeza Kamanda Kuzaga.

Jeshi la Polisi limeendelea kuwasisitiza wananchi kutatua migogoro ya kifamilia kwa njia ya amani na kuepuka kujichukulia sheria mikononi.