MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imedhamini wanafunzi watano wa Kitanzania watakaoshiriki mashindano ya nchi za Afrika ya Hisabati yanayofanyika Chuo Kikuu cha Witwatersland, Afrika Kusini.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari aliyasema hayo juzi wakati anazungumza na waandishi wa habari kuhusu udhamini huo.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya kuendeleza stadi za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) miongoni mwa wanafunzi nchini.
Wanafunzi hao tayari wameshaondoka nchini kwenda Johannesburg, Afrika Kusini ambako mashindano hayo yatafanyika kati ya Agosti 13 na 20 mwaka huu.
Mashindano hayo yanaitwa Olimpiki ya Hisabati Afrika (PAMO). Dk.Bakari alisema taasisi yake imedhamiria kujenga nchi inayowezeshwa kidijitali.
Alitaka wanafunzi na wanazuoni wa Tanzania kupenda masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), ambayo yanajenga misingi imara ya umahiri katika TEHAMA.
"Teknolojia inakua kwa kasi na hivi sasa kuna akili mnemba na programu tumizi nyingi zinazowezesha shughuli nyingi.
"Tanzania inatekeleza mpango wa kubadilisha uchumi wake kuwa wa kidijitali, ambapo TEHAMA inatumika kwenye kila sekta," alisema.
Dk. Bakari alifafanua kuwa, ushiriki wa wanafunzi na wanazuoni katika mashindano yanayoshirikisha wadau ndani ya Bara la Afrika na ulimwenguni kote una umuhimu wa kipekee.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, pamoja kuongeza stadi na kupanua weledi wa washiriki, ushiriki wa vijana hao unatangaza Tanzania na kuijengea nchi taswira nzuri kwenye majukwaa ya kimataifa.
Washiriki wa Tanzania katika mashindano ya PAMO mwaka huu na ambao wanatoka shule za sekondari ni Amborse Rutashobya wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Iyunga; Ilham Abdalla Awadhi wa Feza, Zanzibar; Mwanaarab Said Mbwana wa Sekondari ya Lumumba, Zanzibar; Stella Maliti wa Sekondari ya Wasichana ya Marian na Zakaria Mwita wa Azania.
Mashindano ya PAMO kwa Tanzania yanaratibiwa na Chama cha Hisabati Tanzania chenye makao makuu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. Said Sima, alisema wanafunzi hao watano waliibuka kidedea kwenye mashindano ya kitaifa yaliyohusisha wanafunzi 812 kutoka shule mbalimbali nchini miezi michache iliyopita.
Mlezi wa Kitivo cha Hisabati UDSM, Dk. Sylvester Rugeihyamu, alisema walihangaika kutafuta wafadhili kutoka taasisi mbalimbali, zikiwamo za kiserikali na binafsi hadi TCRA ilipojitokeza.
Alishukuru mamlaka hiyo kuwaunga mkono na kufadhili wanafunzi washiriki wa mashindano hayo, akisema chama hicho peke yake kisingeweza kutuma washiriki wa Tanzania kwenye mashindano ya PAMO bila ya ufadhili wa TCRA, ambayo imetoa tiketi za kwenda Afrika Kusini na kurudi.
Aliomba taasisi nyingine kuiga mfano huo mzuri wa TCRA siku zijazo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED