Trilioni 1.9 zaboresha huduma ya maji Dar,Pwani kwa miaka 4

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:53 AM Mar 11 2025
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Mhandisi Mkama Bwire.
Picha:Nipashe Digital
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Mhandisi Mkama Bwire.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kushirikiana na Serikali imefanikiwa kuwekeza katika utekelezaji wa miradi ya majisafi yenye thamani ya Trilioni 1.19 kwa kipindi cha miaka 4 ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya utekelezaji wa miradi na huduma kutoka DAWASA, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa kati ya miradi hiyo, Bilioni 796.19 ni miradi ya majisafi na miradi yenye thamani ya Bilioni 400.91 ni miradi ya usafi wa mazingira. 

Amesema kuwa kati ya miradi hiyo, miradi iliyokamilika ina jumla ya thamani ya Bilioni 344.67, ambapo, kati ya hiyo miradi ya majisafi ni Tsh. Bilioni 329.97 na miradi ya miradi ya Usafi wa Mazingira ni Tsh Bilioni 14.7. 

Amebainisha kuwa, ipo miradi ya majisafi inayoendelea kutekelezwa katika hatua mbalimbali, ambayo ina thamani ya Bilioni 852.43, ambapo miradi ya majisafi ina thamani ya Bilioni 466.22 na miradi ya Usafi wa Mazingira ina thamani ya Bilioni 386.21. 

Mhandisi Bwire amesema kuwa Mamlaka imefanikiwa kukamilisha baadhi ya miradi mikubwa ya Majisafi ikiwemo mradi wa maji Chalinze Awamu ya Tatu, uliotekelezwa kwa lengo la kusambaza huduma ya maji kwa wananchi wa Mji wa Chalinze, Mboga, Msoga na miono. 

"Mradi umehusisha ujenzi wa vituo 3 vya kusukuma maji vilivyojengwa maeneo ya Miono, Msoga na Mboga. Pia ulazaji wa bomba kwa umbali wa kilomita 923, ujenzi wa matenki 18 ya kuhifadhi maji ya lita 500,000 hadi milioni 2, pamoja na ujenzi wa vioski 330 vya kuchotea maji. 
Mradi unanufaisha wakazi 400,000 wa maeneo ya Miono, Vigwaza, Lugoba, Ubena - Zomozi, Gwata, Mkata, Ngerengere, Manga, Mbwewe na Fukayosi," amesema Mhandisi Bwire. 


Mradi mwingine ambao umekamilika ni pamoja na Mradi wa maji Mlandizi - Chalinze - Mboga ambao umekamilika mwaka 2021 na kunufaisha wananchi zaidi ya 125,000 wa maeneo ya Viwanda vya Tywford, Kiwanda cha ngozi, kiwanda cha Juice Sayona, Stesheni ya Treni ya mwendokasi, Vigwaza, Kijiji cha Mboga, Chamakweza, Chahua - Lukenge, Milo, Ruvu darajani, Mdaula - Ubena Zomozi, Buyuni, Visezi, Pingo, Pera, Bwilingu, Chalinze mjini na Chalinze mzee na Soga. Mradi umetekelezwa kwa gharama ya Bilioni 19.89. 

Serikali imetekeleza na kukamilisha mradi wa usambazaji maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo uliotekelezwa na kugharimu Bilioni 77.9. Mradi ulihusisha ulazaji wa mabomba kwa umbali wa kilomita 1,252, ujenzi wa tenki la maji la lita milioni 5. Mradi umeunganisha wateja 40,000, na kukamilika kwake kumenufaisha wakazi wapatao 450,000 wa maeneo Bagamoyo, Mapinga, Mbweni, Bunju, Wazo, Tegeta A, Salasala, Goba, Mabwepande na Mivumoni. 

Mhandisi Bwire pia aliutaja mradi wa maji Mshikamano ambao umekamilika kwa asilimia 100. Mradi ulihusisha ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji la lita milioni 6, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji, kwa ujumla mradi umegharimu Bilioni 4.8. Mradi umenufaisha zaidi ya wakazi 180,000 wa maeneo ya Mshikamano, Msakuzi, Machimbo na Majengo mapya. 

Mradi mwingine uliokamilika na wenye tija kwa wananchi ni mradi wa maji Kigamboni uliohusisha ujenzi wa tenki kubwa la lita milioni 15, ulazaji wa mabomba kwa umbali wa kilomita 6.35 kwa lengo la kuunganisha wananchi na huduma ya majisafi. Jumla ya wananchi 450,000 wananufaika na kukamilika kwa mradi. 

"Kutokana na mafanikio haya ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya majisafi, imesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uwezo wa uzalishaji maji kutoka kwenye Mitambo ya kuzalisha maji umeongezeka kutoka lita milioni 500,000,000 kwa siku mpaka lita milioni 534,000,000 kwa siku, ambazo ni sawa na ongezeko la lita 34,100,000  kwa siku. Hizi zinahusisha uzalishaji katika Mtambo wa Wami wenye kutoa lita 14,100,000 na visima vya Kimbiji vinavyotoa lita milioni 20,000,000 kwa siku," ameongeza Mhandisi Bwire. 


Ameongeza pia kuwa Mamlaka imefanikiwa kuongeza mtandao wa usafirishaji na usambazaji maji kutoka Kilomita 4,6907 hadi Kilomita 7,206 sawa na ongezeko la kilomita 2,513.4. 

Mhandisi Bwire amebainisha kutokana na hilo, uwezo wa kuhifadhi maji umeongezeka kutoka lita milioni 153,649,000 hadi lita milioni 198,965,000 sawa na ongezeko la lita 45,316,000. Maji yanahifadhiwa katika matenki yafuatayo ya maji Vikawe, Tegeta A, Mshikamano, Mbweni, Bangulo na Kigamboni. 

Mbali na hapo, Mhandisi Bwire amesema kuwa idadi ya maunganisho ya wateja wa majisafi imeongezeka kutoka 343,019 hadi kufikia wateja 455,720 sawa na ongezeko la wateja 112,701. Na kupitia jitihada hizi, tumefanikiwa kukuza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi kutoka wastani wa asilimia 89 hadi asilimia 93 kwa sasa. 

Mamlaka inaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya majisafi kwa lengo kutimiza adhma ya Serikali ya kutoa huduma kwa asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini.