Vijana wahimizwa kuwa karibu na NHIF

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 02:23 PM Mar 11 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dk. Irene Isaka
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dk. Irene Isaka

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dk. Irene Isaka, amesema kwa mujibu wa utafiti ulifanywa 2021/22 imebainika asilimia 22 ya vijana nchini wanakabiliwa na magonjwa yasiyo kuambukiza, ikiwamo magonjwa ya akili.

Amesema, kutokana na hali hiyo vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele, kukata bima ya afya ambayo itawasaidia katika matibabu ya magonjwa hayo.

“Kutokana na hali hii vijana wanapaswa kuwa na bima ili kuwa na uhakika wa matibabu, kwani zamani magonjwa haya yalikuwa yanawakumba watu wenye umri mkubwa lakini hivi sasa vijana wengi ndiyo wanakufa kutokana na magonjwa yasiyo ya kumbukiza,” amesema.

Hata hvyo, amesema bima ya afya inaumuhimu mkubwa sana kwa kila mtu na watu waondokane na dhana kuwa bima ni uchuro.

Pia, amesema kwamba mfuko huo, umeokoa Sh. bilioni 22, katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita, ambacho kilikuwa kinapotea kutokana na udanganyifu wa baadhi ya wanachama.

Dk. Isaka, amesema hayo jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema kutokana na hali hiyo watumishi 36 wa vituo vya kutolea huduma, wamechukuliwa hatua kwa kufanya udanganyifu kwenye mfuko.

Aidha, amesema mfuko hivi sasa una ziada ya Sh. bilioni 95 ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, ulikuwa na nakisi.