Vyama 17 vyakidhi kuwania kiti cha urais Uchaguzi Mkuu

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 07:15 PM Aug 27 2025
 Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Picha: Mpigapicha Wetu
Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Urejeshaji fomu za kugombea urais umekamilika leo katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ambapo mgombea urais kupitia ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, alizuiwa kuingia kutokana na kukosa vigezo.

Kwa mujibu wa kanuni za chama hicho, mgombea wa nafasi ya urais anatakiwa awe mwanachama aliyehudumu ndani ya chama kwa angalau siku 30 kabla ya uteuzi, jambo ambalo Mpina alishindwa kutimiza.

Mpina, ambaye aliwasili saa 6:40 mchana akiwa na mgombea mwenza wake, alizuiwa getini na maafisa wa Tume na kuambiwa wasubiri nje. Hata hivyo, hadi mwisho wa siku, yeye pamoja na wafuasi wake hawakuruhusiwa kuingia ndani kurejesha fomu hizo.

Awali, ACT-Wazalendo walieleza matumaini ya kurejesha fomu hizo ili kujiandaa kuanza kampeni rasmi katika maeneo mbalimbali nchini, lakini walikumbana na kikwazo hicho.

Wagombea wa Vyama Vingine
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, akiwa na mgombea mwenza wake Dk. Emmanuel Nchimbi, walifanikiwa kurejesha fomu zao kwa mujibu wa ratiba ya Tume.

Mbali na CCM, vyama vingine vilivyorejesha fomu ni: NRA, AAFP, Chama Makini, NLD, UPDP, ADA, TADEA, UMD, TLP, CCK, CHAUMMA, DP, SAU, CUF, ADC, UDP, NCCR-Mageuzi na UMD.