Uchaguzi wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) kwa ajili ya madiwani wa viti maalum katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro umeweka historia ya kipekee, baada ya wagombea na wajumbe wake kukesha nje ya Ukumbi wa Tanzanite tangu saa 2:00 asubuhi ya Julai 20 hadi alfajiri ya Julai 21, wakisubiri matokeo kutangazwa.
Matokeo hayo yametangazwa saa 12:15 alfajiri na Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Manispaa ya Morogoro, Khalid King, ambaye pia ndiye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo. Katika matokeo hayo, Mwandishi wa Habari wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Latifa Said Ganzel, ameibuka mshindi wa kwanza kwa kupata kura 934 kati ya wagombea 58 waliowania nafasi hizo.
Latifa, ambaye alikuwa anawania kuendelea na nafasi ya udiwani wa viti maalum aliyoitumikia kwa vipindi viwili mfululizo, ameongoza kwa tofauti kubwa ya kura, akifuatiwa na Batuli Kifea (794), Grace Mkumbae (752), Salma Mbandu (698), na Imakulata Mhagama ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa UWT katika Kata ya Kihonda Maghorofani.
Wengine waliopata kura nyingi ni madiwani waliomaliza muda wao akiwemo Warda Bazia, Rahma Maumba, pamoja na Mwenyekiti wa UWT Kata ya Kihonda, Magreth Ndewe. Vilevile, walikuwapo wagombea wapya waliopata mafanikio kama Amina Kisimbo na Amina Zihuye, ambaye pia alikuwa anatetea nafasi yake.
Hata hivyo, baadhi ya wagombea waliokuwa wakitetea nafasi hizo kwa mara nyingine hawakuweza kupenya katika kumi bora. Miongoni mwao ni Hadija Kibati (maarufu kama Mama Nyau), Aisha Kitime, Zamoyoni Abdallah, na Mwanaidi Ngulungu, ambao kura zao hazikutosha kuwafikisha mbele.
Wakati taarifa za matokeo zikianza kuvuja alfajiri hiyo, wajumbe waliokuwa wamejipanga tangu siku ya uchaguzi walianza kusherehekea kwa bashasha za kimya kimya, wakikumbatiana kwa heshima na mshikamano wa kindugu. “Ni usiku wa kihistoria, wanawake tumeonyesha ustahimilivu mkubwa. Tumekesha kwa heshima ya demokrasia yetu,” alisema Maria Mwakalinga, Katibu wa UWT kutoka Tawi la Kasanga A, Kata ya Mindu.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wagombea waliokosa nafasi walionekana kuondoka kwa utulivu pamoja na wapambe wao, hata kabla ya matokeo kutangazwa rasmi.
Orodha ya majina ya wagombea waliofanikiwa kuingia kwenye kumi bora sasa inatarajiwa kupelekwa kwenye vikao husika vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya mchujo na maamuzi ya mwisho. Iwapo watapitishwa rasmi, idadi yao itaingia kwenye orodha ya wagombea wa viti maalum wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao. Hata hivyo, kama chama hicho kitapoteza nafasi kwenye baadhi ya maeneo, baadhi yao huenda wakaondolewa kwenye orodha hiyo ili kuzingatia uwiano wa kura kitaifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED