WAKILI wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki, Dorice Dario, amesema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ni vema wale wanaotoa maoni wafanye hivyo pasipo kudhalilisha wengine
Amesema Katiba imetoa haki ya kutoa maoni lakini kila kitu kina mipaka yake.
Dorice amesema hayo kwenye banda la Wizara hiyo kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba.
"Wananchi tumepewa haki ya kutoa maoni lakini kila kitu kina mipaka yake, maoni yetu yawe ya busara, yasiwe ya kudhalilisha wengine hasa kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi.
"Haki yetu ya kutoa maoni isitumike vibaya, ili tuweze kuilinda Katiba yetu, tutimize wajibu wetu kama wananchi lakini tulinde Katiba yetu," amesema Dorice.
Kadhalika, amewakumbusha wananchi kwamba katika mwaka huu wa uchaguzi, wanayo haki ya msingi ya kushiriki kuchagua na kuchaguliwa na wasisubiri kukaa pembeni na kulalamika.
"Watu wajitokeze wagombee nafasi mbalimbali na pia wajitokeze kuchagua viongozi wanaofaa kuwaongoza.Katiba imetoa haki ya msingi kwa mwananchi ya kuchagua na kuchaguliwa kwa hiyo endapo hutoshiriki katika eneo hilo tayari utakuwa umejinyima haki ya kupata kiongozi bora.
"Na unapojinyima haki hiyo hatutegemei utoke tena uanze kulalamika kwamba kiongozi fulani hatufai wakati wewe hukushiriki, pengine kura yako moja ingesaidia kumweka madarakani kiongozi anayefaa au yale uliyokuwa ukitumaini yabadilike labda ungeshiriki ungechangia mchakato kuyabadilisha."
Ametoa wito kwa wananchi kwenda kutembelea banda hilo la Katiba na Sheria katika maonesho hayo ili kujifunza mambo mbalimbali ikiwamo kuomba ushauri wa kisheria.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED