Wataalam nchini wakuna vichwa dawa kuzuia kuambukizwa VVU

By Restuta James , Nipashe
Published at 12:27 PM Aug 28 2025
Nembo ya kuondoa unyanyapaa dhidi ya VVU
Picha: Mtandao
Nembo ya kuondoa unyanyapaa dhidi ya VVU

MWEZI mmoja baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuidhinisha matumizi ya dawa ya lenacapavir, inayozuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa miezi sita, wataalamu wa afya nchini, bado ‘wanakuna vichwa’ kuweka utaratibu wa upatikanaji wake.

Lenacapavir iliidhinishwa mwezi uliopita kwenye Mkutano wa 13 wa Sayansi ya VVU wa Jumuiya ya Kimataifa ya UKIMWI (IAS 2025), uliyofanyika jijini Kigali, Rwanda Julai, mwaka huu.

Dawa hiyo inaweza kumkinga mtu dhidi ya maambukizi ya VVU, kwa kuzuia virusi visiongezeke ndani ya seli za mwili katika kipindi cha miezi sita, ikitajwa kuwa njia ya muda mrefu zaidi ya kuzuia VVU na inatarajiwa kugharimu takribani Dola za Marekani 40 kwa mtu kwa mwaka katika nchi za kipato cha chini na cha kati.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu jana, Kaimu Mkuu wa Programu katika Wizara ya Afya, Dk. Samwel Lazaro, alisema wataalamu wa wizara wameshakutana na kuwasilisha mapendekezo kwa Waziri mwenye dhamana ya afya. 

“Wizara imeshapata taarifa kupitia mifumo yake ya ndani inaendelea kulifanyia kazi ili kuona namna bora dawa hiyo inaweza ikapatikana hapa nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, tujue bei na itapatikanaje. Bado tunachakata, tuone ni namna gani itakidhi matakwa ya nchi,” alisema.

Dk. Lazaro alisema mwongozo wa wizara kuhusu matumizi ya dawa, unatoa mwanya wa kuruhusu matumizi ya dawa bora zaidi pale ugunduzi mpya unapopatikana.

“Huwa tunafanya hivi ili tukisikia WHO imeidhinisha na sisi ndani tunaangalia kuhakikisha kuna upatikanaji wa hiyo dawa kwa jamii ambayo nayo ndiyo mnufaika. 

“Tuna taratibu zetu. Hata  kama WHO wameshaidhinisha, ni lazima isajiliwe na TMDA (Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba). Hizi  taratibu bado hazijakamilika, zikikamilika ndiyo tutaona ni namna gani itaanza kupatikana kwa jamii, kwa serikali kununua au wadau,” alifafanua.

“Tumeshaijadili mpaka kwenye kikao cha Mganga Mkuu wa Serikali, lakini anayetakiwa atoe idhini ni Waziri wa Afya, tumeshamwandikia. Nachoweza kukuambia ni kwamba bado tunalichakata,” aliongeza. 

Taarifa ya WHO ya Julai 14, 2025 ilimkariri Mkurugenzi Mkuu wake, Dk. Tedros Ghebreyesus, akisema lenacapavir ndio mbadala bora zaidi kwa sasa, katika vita dhidi ya VVU na kwamba ilikuwa imeonesha mafanikio makubwa katika kuzuia maambukizi yote kwa watu walio katika hatari.

Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa nchi 18 za kwanza barani Afrika kuruhusiwa kuanza matumizi ya lenacapavir, inayotajwa kuwa mwarobaini wa juhudi za kikanda kupambana na virusi hivyo.

Mbali ya Tanzania, nchi zingine zilizoidhinishwa kutumia dawa hiyo ni Kenya, Uganda, Botswana, Eswitini, Ethiopia, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Nigeria, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe.

Takwimu zinaonesha kwamba kuna Watanzania zaidi ya milioni 1.5 wanaoishi na maambukizi ya VVU, ikiwa na maambukizi mapya 60,000 kila mwaka.

Tayari Kenya imetangaza kuweka mkakati wa kuhakikisha dawa hiyo inaanza kupatikana nchini humo Januari mwakani, ikitoa kipaumbele kwa vijana wa rika balehe na wanawake walio katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU.

DAWA NYINGINEZO

Mbali lenacapavir, tayari kuna dawa kinga ya vidonge na sindano (PrEP CAB-LA) na pete kinga inayowekwa ukeni.

Pete kinga hiyo inayojulikana kwa jina la kitaalamu ‘Dapivirine Vaginal Ring (DVR)’, imewekewa dawa maalumu ya kuzuia maambukizi ya VVU, yanayoweza kumpata mwanamke wakati wa kujamiiana.

HALI YA VVU

Takwimu za WHO kwa mwaka jana zinaonesha kwamba watu waliokuwa wakiishi na VVU duniani ni milioni 40.8, huku maambukizi mapya yakiwa watu milioni 1.3, ambao asilimia 65 wako Afrika.

Watu milioni 31.6 wanatumia dawa za kufubaza VVU ikiwa ni ongezeko kutoka milioni 30.3 mwaka 2023.