WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amesema watakaothubutu kuandamana Oktoba 29, watakutana na visiki.
Alisema hayo jana katika mkutano wa kampeni ambazo mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, mjini Karage kwa ajili ya kujinadi kwa wananchi, huku akiahidi mambo kadhaa kwa lengo la kuufungua kiuchumi mkoa wa Kagera na wananchi wake.
Bashungwa ambaye ni mgombea ubunge Jimbo la Karagwe, alipopewa nafasi ya kuzungumza alimweleza Samia kwamba, tangu amempa jukumu la Waziri wa Mambo ya Ndani Ya Nchi, vyombo vya ulinzi na usalama vilivyoko chini ya wizara hiyo, wanaendelea kufanya kazi kwa weledi.
“Wako timamu kwa kushirikiana na vyombo vingine kuhakikisha amani inaendelea kutamalaki. Hakutakuwa na mtu yoyote atakayethubutu kuandamana Oktoba 29, atakutana na visiki,” alisema.
Bashungwa aliwaomba vijana wasikubali kuingia kwenye mkumbo huo kwa sababu wanawapenda na kuwaomba waungane na mgombea wa urais kwa sababu ilani ya uchaguzi imesheheni mambo mazuri ya maendeleo.
AHADI ZA SAMIA
Katika mikutano yake mitatu iliyofanyika jana akianzia Muleba, kisha Missenyi na kumalizia Karagwe, Samia aliendelea kutoa ahadi atakavyowezesha kukuza uchumi na kubadilisha mkoa kuwa na fursa za kiuchumi na kimbilio la uwekezaji.
Akiwa Missenyi, aliahidi ujenzi wa kiwanja cha ndege eneo la Kyabajwa ambao utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa Boeing 373-9 zenye uwezo kuchukua abiria 180-220.
Samia pia aliahidi kutupia jicho vanilla ili kuitangaza Tanzania duniani kuwa inalizalisha zao ambalo soko kubwa linategemewa duniani kwa asilimia 75 ni Madagascar ikifuata Uganda.
Samia aliwaeleza wana Missenyi kuwa daraja la Kyaka lenye historia ya vita vya Kagera ni alama ya uwezo wa Tanzania kujilinda na kizuizi cha kijografia katika mapambano.
“Ni alama ya uwezo wa Tanzania wa kuinuka na kujenga upya, ambapo ndio falsafa ya R4 kwa serikali ya awamu ya sita. Ahadi yangu ni kudumisha umoja, kulinda uhuru, amani na utulivu nchini,” aliahidi Samia.
Alisema Idd Amini alivunja daraja hilo kuzuia majeshi ya Tanzania kwenda Uganda kumpiga, lakini jeshi lilimkabili na kumwondoa madarakani.
“Baada ya vita lilijengwa na sasa ni kiungo muhimu cha biashara na uchumi na ni alama,” alisema.
Ahadi zingine alizotoa kwa wananchi hao ni kujenga miradi tisa ya maji, miundombinu ya barabara na kukamilisha daraja la Kitengule ambalo ni kiungo cha wilaya za Missenyi, Karagwe na Ngara lenye urefu wa mita 140 na barabara unganishi urefu wa kilometa 18 kwa Sh. bilioni 31.5.
Pia aliahidi kukamilisha chuo cha VETA Buyango na ujenzi wa soko la kisasa, kupeleka miche milioni mbili ya kahawa na ya parachichi 500,000.
AHADI MULEBA
Samia aliahidi kukuza zao la kahawa kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora Bora (BBT) na kuwapatia boti za uvuvi, za kubeba wagonjwa na za kudhibiti uvuvi haramu Ziwa Victoria unaochangia upungufu wa samaki.
Alisema wanafahamu mkoa huo ni wa kilimo cha kahawa, migomba na pia uvuvi na ufugaji na kwamba kwa miaka mitano serikali ilielekeza jitihada katika kuzivuta sekta za uzalishaji ikiwamo ujenzi wa miundombinu usafiri na usafirishaji na huduma za jamii.
Miaka mitano iliyopita, alisema walianzisha mashamba makubwa ya kahawa na migomba, likiwamo shamba la ekari 300 lililoko kijiji Makombora na vijana 300 wanaendelea na shughuli hizo kupitia (BBT).
Alisema programu hiyo imekwenda pia katika sekta ya madini ili kuwajengea kesho iliyo bora vijana na mkoani kagera inafanyika kwa ajili ya kuzalisha kahawa.
Samia alisema watakapopewa ridhaa wataongeza uzalishaji wa miche ya kahawa na kuwezesha upatikanaji wa matrekta ili kurahisisha shughuli hizo pamoja na kuendelea sera ya kutoa ruzuku ya pembejeo ili uzalishaji uwe mkubwa.
Katika kuendeleza kongani za viwanda, alisema wataliangalia suala la usindikaji wa mazao ya uvuvi na kuongeza boti za kisasa zitakazotolewa kwa mikopo.
Pia alisema baada ya kuboresha mfumo wa utoaji mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri, vikundi vilivyonufaika huko ni 152 vilipatiwa Sh. bilioni 2.2 iliyochangia kuwaongezea kipato cha mtu mmoja mmoja.
Alitaja mambo yanayohitajika kufanyiwa kazi kupitia ilani 2025/2030 kuwa ni pamoja upungufu wa vyanzo vya maji vya uhakika mkoani Kagera hasa wilaya ya Muleba ambako hutegemea mito na visima visivyo vya uhakika.
Aidha, alisema serikali imefanya usanifu kupitia Ziwa Victoria, ambayo kwa miaka kadhaa hawajayatumia maziwa hayo vyema. Alisema anatambua uhitaji wa usafiri wa uhakika Ziwa Victoria kwa ajili ya abiria, mazao ya uvuvi na kilimo.
Kadhalika alisema kumekuwa na tatizo la usafiri wa wagonjwa kwa wakati, hivyo kuahidi boti mbili za kusafirisha wagonjwa wa kata Goziba na Bumbire na kujenga gati mbili Kituo na Mrumo.
Aliahidi pia kuwapatia boti tatu za doria ili kuangalia usalama na kudhibiti uvuvi haramu unaochangia upungufu wa samaki ndani ya Ziwa Victoria.
Katika mkutano wa Karagwe, Samia alitaka matayarisho ya kupiga kura Oktoba 29, yaanze sasa kwa kila mtu kujua kituo chake na amepangwa wapi ili siku ya kura wajue.
SAMIA ANAKUBALIKA
Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, alisema umati katika mikutano hiyo ni kiashiria cha mgombea urais kukubalika na Watanzania na wana matarajio makubwa kwake.
Naye kada mpya wa CCM, Ezekia Wenje, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Victoria, alisema alichojifunza na analojua ni kuwa kiongozi wajibu wake mkubwa ni kutoa tumaini kwa anaowaongoza.
VIWANDA VYA ALIZETI
Mgombea Mwenza wa Urais kupitia CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema miaka mitano ijayo endapo watashinda Uchaguzi Mkuu, watahakikisha kunajengwa viwanda vya kusindika mafuta ya alizeti mkoani Singida, ili kupunguza utegemezi wa kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.
Alitoa ahadi hiyo jana wilayani Ikungi katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.
Dk. Nchimbi alisema maendeleo ya viwanda yatakuwa nguzo kuu katika mpango wa miaka mitano wanauchumi wa CCM, huku uzalishaji wa mafuta ya alizeti ukitambuliwa kama ajenda ya kitaifa ya kuongeza uzalishaji wa ndani na kujitegemea.
Balozi Nchimbi aliongeza kuwa mbali na uchakataji wa mafuta, viwanda hivyo vitaunda mnyororo kamili wa thamani kwa kujenga viwanda vya kutengeneza chakula cha mifugo kwa kutumia mabaki ya alizeti, hatua itakayosaidia sekta ya mifugo na kuimarisha usalama wa chakula.
Alisema ahadi hiyo inaendana na malengo mapana yaliyobainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, inayosisitiza uanzishwaji wa viwanda vya kusindika mazao, nyama na maziwa kama sehemu ya mkakati wa kuendeleza kilimo-biashara na kuchochea uchumi wa vijijini pamoja na kupanua ajira.
Aidha, alitaja hatua kuu zitakazowezesha mafanikio ya mpango huo, ikiwamo kuongeza upatikanaji wa mbolea na mbegu bora kupitia ruzuku, kuendeleza miradi ya umwagiliaji ili kuruhusu kilimo cha mwaka mzima na kuboresha miundombinu ya kuhifadhia mazao baada ya mavuno.
Ahadi ya ujenzi wa viwanda vya mafuta ilipokewa kwa furaha na wakazi pamoja na wakulima wa eneo hilo, ambao walisema fursa ya muda mrefu ya kuongeza thamani ya mazao yao na kuendeleza uchumi wa mkoa huo.
AHADI SAU
Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Sauti ya Umma (SAU), Majaliwa Kyara, amewataka wakazi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla kufanya mabadiliko ya kweli kwa kuchagua chama hicho, akisisitiza kuwa wakati umefika wa kujikomboa kiuchumi na kijamii.
Akizungumza katika moja ya mikutano yake ya kampeni mkoani Arusha, Kyara alisema endapo atapewa ridhaa ya kuiongoza nchi, serikali yake itahakikisha upatikanaji wa bima za afya kwa wananchi wote, pembejeo za kilimo kwa bei nafuu, na elimu bora bure kwa wanafunzi nchini.
“Tutahakikisha kila kata nchini inapata maji safi na salama, kwa sababu huduma ya maji ni haki ya msingi, si anasa,” alisema Kyara .
Katika sera zake, SAU imeeleza dhamira ya kuwasaidia wakulima na wafugaji kwa kuondoa changamoto za masoko na kuwezesha uongezaji thamani wa mazao na bidhaa za mifugo, hatua itakayoongeza ajira na kipato kwa wananchi.
Katika kampeni zake mkoani Arusha, wagombea hao wa SAU wametembelea majimbo ya Arusha Mjini, Arumeru Magharibi na Arumeru Mashariki, wakijipatia uungwaji mkono kutoka kwa wananchi.
Imeandikwa na Romana Mwallya, KARAGWA, Gwamaka Alipili, IKUNGI na Godfrey Mishi, ARUSHA.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED