Naibu Meneja Mkuu wa Kampuni ya The Guardian Ltd (TGL) inayochapisha magazeti ya The Guardian na Nipashe, Jackson Paul (wa pili kulia), akim-karibisha Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Saleh Saad Mohamed.
Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imeandaa Kongamano la Uwekezaji la mwaka 2025 (Zanzibar Investment Summit 2025) litakalofanyika eneo la Micheweni, kisiwani Pemba, kwa lengo la kuonesha fursa mpya na lukuki za uwekezaji zinazopatikana katika kisiwa hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari wa Nipashe alipokuwa akitembelea ofisi za Kampuni ya The Guardian Limited, Mikocheni jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Saleh Saad Mohamed, amesema kongamano hilo linatarajiwa kufanyika kuanzia Mei 7 hadi 10, 2025.
Kwa mujibu wa Mohamed, kaulimbiu ya kongamano hilo ni "Ni Wakati wa Pemba" (It’s Time for Pemba), likiwa na lengo kuu la kukifungua kisiwa cha Pemba kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Kongamano hilo linatarajiwa kuwavuta wawekezaji zaidi ya 1,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani.
“Hili ni lengo mahsusi la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar – tunataka kukifungua kisiwa cha Pemba. Zanzibar ni eneo lenye fursa nyingi sana za uwekezaji. Wengi wamekuwa wakiifikiria Unguja pekee, lakini ukweli ni kwamba Pemba, hususan eneo la Micheweni, lina fursa kubwa sana kwa wawekezaji,” amesema Mohamed.
Aidha, ameeleza kuwa wakati wa kongamano hilo, wawekezaji watapewa nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali muhimu yenye fursa za uwekezaji kisiwani humo.
“Kutakuwa na matukio matatu makuu. Siku ya kwanza kutafanyika michezo mbalimbali kwa ajili ya kujenga urafiki na kufahamiana zaidi kati ya wadau. Wadau pia wanakaribishwa kuleta misaada mbalimbali ya kurejesha kwa jamii (CSR) – chochote mtu alichonacho anaweza kuleta kuwasaidia wanajamii,” amebainisha.
Mohamed ameongeza kuwa siku ya pili itakuwa ni ya kongamano rasmi ambapo wawekezaji 1,000 kutoka kote duniani watakutana kwa chakula cha jioni na viongozi wakuu wa serikali, pamoja na kutoa nafasi kwa kila mmoja kueleza kazi na miradi wanayoifanya. Pia, kutakuwa na maonesho ya shughuli na bidhaa za kampuni mbalimbali kwa siku zote za kongamano hilo.
Alizitaja baadhi ya sekta zenye fursa za uwekezaji kisiwani Pemba kuwa ni pamoja na:
🌊 Uchumi wa buluu kutokana na uwepo wa mazao mengi ya baharini;
🏠 Ujenzi wa nyumba za makazi;
💉 Sekta ya afya;
⚓ Bandari katika maeneo ya Wete, Wesha na Koani kwa ajili ya kukuza usafirishaji wa majini;
🏖️ Utalii, ujenzi wa hoteli, pamoja na mazao ya karafuu na mwani.
Kwa mujibu wa Mohamed, serikali imeanza kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara kwa ajili ya kuunganisha maeneo mbalimbali ya Pemba ili kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji. Tayari wakandarasi wameanza kazi katika maeneo husika.
Kuhusu ushiriki wa kongamano hilo, Mohamed amesema wanatarajia wageni kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, huku akibainisha kuwa tayari baadhi yao wamejisajili kupitia tovuti rasmi ya kongamano hilo: www.zis.co.tz.
“Tunaishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na ofisi za balozi zetu katika nchi mbalimbali kwa kulibeba suala hili na kulitangaza. Mwitikio ni mkubwa sana. Wapo waliothibitisha ushiriki na wengine wanaendelea kujiandikisha. Huu utakuwa mkutano mkubwa wa kwanza wa uwekezaji Zanzibar,” ameeleza.
Aidha, amesema ZIPA ipo katika mazungumzo na watoa huduma za usafiri wa anga na majini ili kuwezesha huduma hizo muhimu kwa washiriki. Kwa wale watakaopenda kushiriki katika mashindano ya mbio za marathoni, serikali imepanga kugharamia usafiri wao hadi eneo la tukio.