WABUNGE leo watapokea mapendekezo ya serikali ya kiwango cha ukomo wa bajeti na mpango wa Mwaka 2025/26.
Bajeti ya mwaka 2024/25 ilikuwa ni Sh. trilioni 49.3.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Ofisi ya Bunge, Waziri wa Fedha, Dk.Mwigulu Nchemba ataeleza mapendekezo ya serikali ya bajeti ya 2025/26 inatarajiwa kukusanya na kutumia.
Pia, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo atawasilisha mapendekezo ya mpango kwa mwaka huo.
Baada ya mkutano huo, kamati ya bajeti itafanya ziara katika mgodi wa dhahabu ya North Mara kisha kufanya uchambuzi wa mapendekezo ya mpango na ukomo huo wa bajeti ya serikali kwa Mwaka 2025/26.
Pia, Kamati 11 za kisekta zitatembelea na kukahua utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotengewa fedha kwa mwaka 2024/25.
Pamoja na kamati hizo Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitatembelea miradi iliyokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa lengo la kufuatilia matumizi ya fedha za umma kwenye miradi hiyo.
Kadhalika, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), itatembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya uwekezaji wa mitaji ya umma kwa lengo la kubaini iwapo utekelezaji wa miradi hiyo ya uwekezaji una ufanisi na kwamba umezingatia sheria, taratibu na miongozo ya biashara.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilieleza kuwa baada ya ziara ya kamati hizo 11 na kamati ya Bajeti zitachambua taarifa za wizara kuhusu utekelezaji wa Bajeti 2024/25 na makadirio ya mapato na matumizi kwa Mwaka 2025/26.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED