UJENZI wa taifa unahitaji mchango wa kila Mtanzania bila kujali tofauti za kisiasa, dini, jinsi na ukanda.
Kwa kuzingatia hilo, Rais Samia Suluhu Hassan, anasisitiza umoja wa kitaifa ili Watanzania washiriki kwa uhuru katika ujenzi wa nchi yao kupitia maarifa, mawazo, elimu na shughuli za kiuchumi wafanyazo.
Akiona umuhimu huo wa ujenzi wa taifa kwa pamoja, Rais anasimamia falsafa ya R4 ambazo zinatafsiriwa Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reform (Mabadiliko) na Rebuiding (Kujenga upya).
Maridhiano ni muhimu katika ujenzi wa taifa ili kuwa na sauti moja, kwani maelewano yanawezesha kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa umoja, amani na kukosoana.
Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wanasema, falsafa hiyo ya Rais inaweza isifanikiwe iwapo matukio ya yanayoendelea sasa ya utekaji wa watu na mauaji vitaendelea bila kuchukuliwa hatua madhubuti ya kuvidhibiti.
Katika mazungumzo yake na gazeti hili, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha CUF Bara, Magdalena Sakaya anasema, yanayotokea sasa ni kama hizo 4R za Rais hazina maana.
"Matukio haya ni kwamba kuna kadhaa ninayoyaona. Kwanza Rais, hajagundua kinachoendelea au kuna watu wanamzunguka ama kuna watu ndani ya serikali wanamzunguka," anasema Magdalena.
Naibu katibu mkuu huyo anasema, ni wakati sasa Rais kusimamia 4R zake kwa vitendo, kwa maelezo kwamba inawawia vigumu Watanzania kujua ni nani anaagiza matukio ya utekaji na kuua watu.
"CUF tumepokea kwa mshtuko taarifa ya kuuawa kwa Mjumbe wa Sekretarieti Kuu ya (CHADEMA), Ali Mohamed Kibao. Matukio ya watu kupotea na kukutwa wameuawa yanaanza kujirudia," anasema.
Anasema, Rais ana nia ya kweli ndio maana alianzisha falsafa hiyo na kuunda Tume ya Haki Jinai, inayogusa haki ya kwanza binadamu ambayo ni kuishi, na kwamba anashangaa kuona yanakuwapo matukio yanayokwenda kinyume na falsafa na haki ya kuishi.
Anatoa wito kwa serikali kushughulikia tatizo hilo ambalo anasema linatengeneza hofu na kuirudisha nchi katika maisha ya taharuki na kuwafanya watu kuishi pamoja kwa upendo na kuaminiana.
AIBU KWA TAIFA
Mwenyekiti wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (CEGODETA), Thomas Ngawaiya, anasema, matukio hayo ni aibu kwa taifa lenye amani na utulivu na ni kikwazo kwa falasa ya Rais.
"Tumemsikia Rais akisema anataka taarifa za matukio hayo haraka, nasi tunaomba uchaguzi usizidi wiki mbili, ikiwezekana, waitwe wachunguzi wa kimataifa kama CIA ya Marekani kusaidia kuchunguza," anashauri Ngwaiya.
Anafafanua kuwa vyombo vya uchunguzi vya Tanzania vipo, lakini matukio yanazidi kuongezeka na kuongeza kuwa njia nzuri ni kuongeza wachunguzi kutoka nje ili ukweli ujulikane.
Mwenyekiti huyo anasema, uchunguzi ukikamilika, watangazwe hadharani ili watu wawajue na iwe fundisho kwa wengine ambao wamekuwa wakiteka watu na kuchafua taswira ya nchi na kusababisha hata wageni kuwa na mashaka usalama wa maisha yao wawapo nchini.
"Kuishi ni haki ya kikatiba ya kila mtu, hakuna mtu mwenye ruhusa ya kutoa uhai wa mwingine. Sisi CEGODETA tunafuatilia ili kuona haki inatendeka, asiwepo wa kuonewa katika uchunguzi huo, na ni vyema ukafanyika kwa muda wa wiki mbili," anasema.
UPINZANI KWA RAIS
Kada wa CCM ambaye ni mchambuzi wa siasa, Abdulkarim Atiki, anasema, matukio ya kuteka na kuua watu yanafanywa na wale wanaopinga falfasa ya Rais Samia.
"Hao ni wale wanaoendekeza siasa za ubabe tulizoshuhudia zaidi ya miaka sita iliyopita, Rais amejitahidi kuwaunganisha Watanzania, lakini anakutana na upinzani," anaonya Atiki.
Anasema, mtu akitaka kutenda haki kwa wananchi ni lazima atakutana na upinzani, na kwamba hata Rais anakutana nao kwa njia hiyo ya matukio ambayo inalenga kumchafua mbele ya jamii.
Anafafanua kuwa kiongozi wa nchi anataka mgombea anayeshinda katika uchaguzi apewe haki yake, na kwamba ndio maana ameruhusu kuwapo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
"Ukiniuliza kuhusu matukio yanayoendelea, nitayaita upinzani kwa Rais unaofanywa na wasiomtakia mema, lakini ninamtia moyo aendelee kuchapa kazi kuunganisha Watanzania," anasema.
Mchambuzi huyo wa siasa anasema, uongozi wa Rais Samia umepoza machungu ambayo Watanzania walikuwa nayo kuanzia mwaka 2015 hadi mwanzoni mwa mwaka 2021, wakati wa awamu ya tano.
"Katika siasa, wapo baadhi ya watu wana mihemko, hawa wanatakiwa kupelekwa katika vyuo maalum ili wakafundishwe jinsi nchi inavyoongozwa, badala ya kuonyesha ubabe.
UKIMYA NI CHANZO
Mwanachama wa CHADEMA, Suzan Lyimo anasema, ukimya wa vyombo vya dola ni chanzo cha matukio hayo na kufafanua kuwa falsafa ya R4 na kuifanya ikose maana kama matukio hayo ndani ya jamii.
"Kuna kauli zilizowahi kutolewa na baadhi ya makada wa CCM za kutishia kupoteza watu, lakini viongozi wa chama hicho walisikika wakiwakana, lakini vyombo vya dola vikawa kimya," anakumbusha Suzan.
Anasema ukimya huo wa vyombo vya dola umetengeneza hofu na kuirudisha nchi enzi za vitisho, taharuki na kila aina ya vitendo vya ukatili ambavyo havikubaki ndani ya jamii iliostaarabika.
"Ni vyema Rais akajitokeza mwenyewe na kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu matukio hayo ambayo yanaenda kinyume na falsafa yake ambayo inalenga kuwaunganisha Watanzania," anasema.
Suzan anasema, matukio ya kuteka na kuua watu yanapaswa kulaaniwa na watu wote wakiwamo viongozi wa dini, si wanasiasa tu, pia kuhakikisha waliohusika wanakamatwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED