Katika jitihada za kupunguza vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na uzazi, wataalamu wa afya nchini wameendelea kubuni njia mpya za utoaji huduma bora za uzazi.
Mojawapo inayochukua nafasi sasa, ni ya huduma ya kujifungua inayotajwa kufanywa ndani ya maji, ambayo sasa imeanza kutolewa katika baadhi ya hospitali nchini, hata kuonekana kuwa na manufaa makubwa kwa mama na mtoto.
Agnes Ndunguru ni mkunga mtaalamu, anayesema huduma hiyo imeshafanyiwa utafiti zaidi ya miaka 40 na kuonekana ni mkombozi kwa afya ya mama na mtoto wakati wa kujifugua.
Anasema nchini, huduma hiyo ina miaka mitatu na kwamba yeye ndiyo mwanzilishi, tayari wameshahudumia wajawazito zaidi ya 200, wote wakijifungua salama na watoto wao kuwa na afya njema.
“Huduma hii faida yake mama anakuwa na amani wakati wa kujifungua, kwa sababu maji yanakuwa na vuguvugu, homoni zake kumwagika kwa wingi mwilini, na kumsaidia kujifungua kwa njia ya kawaida, pia kupungua hatari ya kuchanika uke,” anasema Ndunguru.
Anafafanua kwamba kwa mtoto, humsaidia kumkinga na uzito uliokithiri, kumpunguzia hatari ya kuugua kisukari, kupata “arrege” na kutolazwa baada ya kuzaliwa, sababu inapunguza hatari ya kupata matatizo ya upumuaji.
“Huduma hii haina madhara kwa mtoto, kwa sababu mtoto akiwa tumboni mwa mama yake miezi tisa huwa anaishi kwenye maji.
“Kwa hiyo hata akizaliwa ndani ya maji ambayo yana joto maalumu, atahisi bado yupo kwenye tumbo la mama yake,” anafafanua Mkunga Ndunguru.
Anasema mtoto akishatolewa ndani ya maji na kuletwa juu, muda wa sekunde mbili ndipo ataanza kupumua au kulia na kwamba akitolewa tu kwenye maji hayo, hapaswi kurudishwa tena kwa sababu itamletea matatizo.
Mkunga anaeleza kuwa, huduma hiyo inatolewa kwenye hospitali mbalimbali ambazo wakunga na wataalamu wameshapatiwa mafunzo hayo, ikiwamo Hospitali ya Taifa Muhimbili (NMH).
MKUNGA MUASISI
Katika maadhimisho ya Siku ya Mkunga Duniani Mei 5 (Jumatatu wiki hii) mwaka huu ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Shinyanga, Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kilimtunuku Tuzo Mkunga Agnes, kutokana na ubunifu wake wa kuzalisha wajawazito hapa nchini ndani ya maji na kupunguza vifo vya uzazi.
Rais wa TAMA, Dk. Beatrice Mwilike, anasema chama hicho kina wanachama zaidi ya 5,000 na kwamba wakunga hao huchangia kwa asilimia 87 katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Hapo anaiomba pia serikali iendelee kuboresha huduma bora za afya, pamoja na kuajiri wakunga wengi, kwa sababu bado kuna upungufu wao, hasa katika ngazi ya zahanati.
Mkurugenzi wa Huduma za Ukunga na Uuguzi kutoka Wizara ya Afya Saturini Manangwa, anasema zaidi ya asilimia 90 ya huduma za mama na mtoto hutolewa na wakunga, na katika hilo anawasihi waendelee kutoa huduma zenye ubora, pamoja na kufuata maadili wakizingatia viapo vyao.
RC & RMO SHINYANGA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, anaungana na wataalamu hao wa afya, na kuwasihi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi, ili kufikia malengo ya serikali ya kupunguza vifo vya uzazi kufika 70 kwa vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.
Anasema bila jitihada zao, serikali haiwezi kufikia malengo hayo ya kupunguza vifo vya uzazi zaidi, licha ya kwamba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa akiboresha huduma za afya pamoja na kununua vifaa tiba vya kisasa.
“Nawaomba wakunga endeleeni kuwa wabunifu katika utoaji wa huduma hizi za uzazi na kupunguza vifo vya mama na mtoto, malengo ya serikali hadi kufika 2030 vifo hivi vipungue hadi 70 kwa vizazi hai 100,000,” anasema Mkuu wa Mkoa Macha.
Anawasihi, pia wajawazito kujenga tabia ya kupenda kujifungua kwenye huduma rasmi za afya, sehemu ambazo kuna wataalamu wa afya na vifaa tiba vya kutosha, ili wajifungue salama na kupunguza vifo vya uzazi.
Lingine Mkuu wa Mkoa analitaja ni takwimu za wajawazito kujifungua kwenye huduma za afya, kwamba zimeongezeka kutoka asilimia 63 mwaka 2016, hadi asilimia 81 Aprili mwaka huu.
Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na viashiria vya Malaria (THDS) ya mwaka 2022, inaonyesha kwamba vifo vya uzazi vimepungua.
Inarejea mfano wa mwaka (2015/2016) kulikuwa na vifo 556 kwa vizazi hai 100,000, lakini vimepungua hadi vifo 104 kwa vizazi hai 100,000.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Yudas Ndungile, anasema, kupungua kwa vifo hivyo ni mafanikio ambayo yametokana pia na wakunga, pamoja na maboresho makubwa katika sekta ya afya ambayo yamefanywa na serikali.
Anatoa mfano kwa mkoa kwake Shinyanga, kwamba serikali imejenga hospitali mpya nne na kukarabati hospitali mbili kongwe, ikiwamo ya Manispaa ya Shinyanga, vilevile kujenga vituo vipya ya afya 18.
Ni hesabu inayofika mbali kwa kuajiri watumishi wa afya 920, kununua vifaa tiba vya kisasa na sasa wanajenga ‘Jengo la Huduma ya Mama na Mtoto’ lililofika kiwango na limefika asilimia 86.
MKAZI SHINYANGA
Mwanamke Jesca Titus, mkazi wa Shinyanga, katika maoni yake anasema huduma hiyo ya kujifungua ndani ya maji ndiyo kwanza anaisikia.
Rai yake ni kwamba ifikishwe katika hospitali za mikoa mbalimbali na kutolewa elimu ipasavyo, kwa sababu anahisi kuwa nzuri zaidi, ambayo itawaepusha pia wanawake kujifungua kwa njia ya upasuaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED