Simbu atoboa siri kutwaa medali ya kwanza ya dhahabu

By Sanula Athanas , Nipashe
Published at 03:39 PM Sep 15 2025
Simbu atoboa siri kutwaa medali ya kwanza ya dhahabu

Katika moja ya ushindani mkali kuwahi kushuhudiwa kwenye mashindano ya dunia ya marathon, Alphonce Simbu ameandika historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya riadha, baada ya kushinda mbio za marathon kwa wanaume kwa tofauti ndogo zaidi katika historia ya mashindano hayo.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 33 alikata utepe mbele kidogo ya Amanal Petros kutoka Ujerumani, katika kile kinachoitwa "photo finish" – ushindi uliotolewa kwa msaada wa picha kutokana na ukaribu wa kumaliza.

Muda rasmi kwa wote wawili ulikuwa 2:09:48, lakini Simbu aliibuka mshindi kwa tofauti ya sekunde 0.03 tu. Iliass Aouani kutoka Italia alishinda medali ya shaba kwa muda wa 2:09:53.

KAULI YA SIMBU
"Si kuandika tu historia, nimefungua ukurasa mpya kwa Tanzania," amesema Simbu kwa furaha baada ya ushindi wake mkubwa.

"Ninakumbuka mwaka 2017 pale London niliposhinda (medali ya) shaba. Nimejaribu mara nyingi tangu hapo bila mafanikio, lakini leo nimepata kile nilichokitafuta kwa muda mrefu.

"Nilipofika hapa, niliambia nafsi yangu kwamba siwezi kukata tamaa. Nilikaa na kundi hadi mwisho, na mbinu hiyo imenisaidia. Angalia tu jinsi nilivyokimbia mita za mwisho."

Ushindi huu si tu wa kwanza kwa Simbu binafsi, bali ni wa kihistoria kwa taifa zima la Tanzania katika michezo ya riadha ya kimataifa. ni medali ya kwanza ya dhahabu kwa Tanzania katika mashindano ya dunia ya riadha (World Athletics Championships).

USHINDANI MKALI
Amanal Petros kutoka Ujerumani, licha ya kukimbia kwa kasi ya kushangaza na kulala chini akiwa amejifunika na utepe wa kumalizia mbio, ilibidi aridhike na medali ya fedha.

"Hii ilikuwa kama mbio za mita 100," amesema Petros baada ya pambano hilo kali. "Nilikuwa ninafikiria ushindi, na kwa kweli kuna huzuni kidogo. Lakini ninapaswa kukubali. Kama mwanariadha, unajifunza kila siku – unajiandaa kwa kesho, unajitahidi zaidi na kushukuru kwa fedha hii."

MASHUJAA WENGINE
Iliass Aouani kutoka Italia ameonesha uwezo mkubwa kwa kumaliza katika nafasi ya tatu, akitumia 2:09:53, muda uliokuwa karibu sana na washindi wawili wa kwanza.

Hadi kufikia kilomita ya 30, kundi kubwa la wakimbiaji lilikuwa pamoja, likiwa na wanariadha waliokuwa kwenye orodha ya waliotarajiwa kushinda, wakiwamo Abel Chelangat wa Uganda, Clayton Young wa Marekani na Emile Cairess wa Uingereza.

Tofauti kati ya wakimbiaji 12 wa mbele ilikuwa ni sekunde chache tu – ishara ya ushindani mkali uliokuwapo.

Lakini hali ya hewa ya joto na unyevunyevu ilianza kuchukua nafasi katika hatua za mwisho, na baadhi ya wakimbiaji wakaanza kushindwa kuhimili kasi.

Kondo Ryota, mshindani anayependelewa na wenyeji wa Japan, alionesha ushupavu kwa muda mrefu lakini alipunguza kasi alipokimbia kilomita ya 39, hatimaye akamaliza katika nafasi ya 11.

BALAA LA KUMALIZIA
Mashabiki walilipuka kwa shangwe walipowaona wakimbiaji wakiingia katika Uwanja wa Taifa wa Japan kwa hatua ya mwisho ya mbio hizo – baada ya kukimbia kilomita 42.195 katika mazingira ya joto la hadi nyuzi 27 za Celsius.

Katika mita kumi za mwisho, Simbu alionesha nguvu ya ajabu ya "kupiga hatua", akijitutumua hadi kumshinda Petros kwa tofauti ndogo zaidi kuwahi kutokea kwenye marathon ya dunia.

MWAKA BORA KWA SIMBU
Mwaka huu umeonekana kuwa wa mafanikio makubwa kwa Simbu. Mbali na ushindi huu wa kihistoria Tokyo, alishika nafasi ya pili kwenye Boston Marathon 2025 mwezi Aprili – tukio lingine kubwa la marathon duniani.

Kwa sasa, Simbu si tu anakuwa na medali ya shaba ya mwaka 2017, bali pia anajiunga kwenye orodha ya mabingwa wa dunia waliotoka barani Afrika, na pia kuwa chachu ya kuamsha ari kwa wanariadha chipukizi wa Tanzania.

Ushindi wake unaibua matumaini mapya kwa mchezo wa riadha Tanzania, ambao kwa miaka mingi umekuwa ukiishi kwenye kivuli cha majirani zake – Kenya, Ethiopia na Uganda.

Simbu amevunja ukuta wa kimya, na kufungua ukurasa mpya kwa wanariadha wa Tanzania. Mafanikio yake yanaweza kuwa kichocheo kwa serikali, mashirika ya michezo na wadau mbalimbali kuwekeza zaidi katika vipaji vya ndani.