Timu ya Azam FC inatarajiwa kushuka dimbani kesho kuvaana na JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu NBC Tanzania Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo, Dar es Salaam.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, hasa ikizingatiwa kuwa katika msimu uliopita timu hizo zilitoka suluhu ya kutofungana.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Flerent Ibenge, akizungumza na waandishi wa habari leo, amesema kikosi chake kimekamilisha maandalizi na wachezaji wote wako na morali ya juu kuelekea mchezo huo.
"Kwa upande wangu sina presha na mchezo huo licha ya kuwa JKT ni timu nzuri. Nitacheza kwa furaha kwa sababu napenda mpira," amesema Ibenge.
Kwa upande wake, mchezaji Feisal Salum, akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, amesema kikosi cha Azam kipo tayari kwa ushindi.
"Kwa upande wetu sisi wachezaji tumejipanga vizuri kuhakikisha tunapata pointi tatu. Tunafahamu wapinzani wetu wana wachezaji wazuri na ushindani, lakini hatuna wasiwasi," amesema Feisal.
Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amesema wanaiheshimu Azam kutokana na ubora wa wachezaji wake na benchi la ufundi, lakini lengo lao ni kushinda.
"Ninaiheshimu Azam kwa kuwa ni miongoni mwa timu bora nchini, hivyo tutaingia kwa tahadhari kubwa ili tuweze kupata pointi tatu," amesema Ally.
Ameongeza kuwa wachezaji wake wote wapo vizuri isipokuwa Said Hamisi ambaye ni majeruhi, huku akiweka wazi kuwa makosa yaliyokuwa yanafanyika katika michezo iliyopita yamerekebishwa.
Kwa upande wake, mchezaji Jafari Maneno amesema:
"Tutafuata maelekezo ya mwalimu ili tupate ushindi. Tunaamini ni mchezo mgumu, hivyo tunaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED