Fadlu: Kipigo hakitatutoa kwenye malengo yetu

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:33 AM Sep 18 2025
news
Picha Mtandao
Wachezaji Kibu Denis wa Simba (kulia) na Shadrack Boka, wakiruka juu kuwania mpira kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa juzi kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

WAKATI kikosi cha Simba kikiondoka nchini jana kwenda Botswana kwa ajili ya mchezo wao wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha wa timu hiyo Fadlu Davids, amesema matokeo waliyoyapata kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii hayatawatoa kwenye malengo yao ya msimu huu.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Fadlu, alisema kipigo cha bao 1-0 walichokipata kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga kimewaumiza lakini kwa sasa wanaangalia kilichopo mbele na bado malengo yao ya msimu yapo palepale.

"Ulikuwa mchezo wa hisia, nafahamu mashabiki wetu wameumia kwa matokeo haya, lakini tunapaswa kuangalia malengo yetu, Simba inaweza kufanya vizuri kwenye michezo ijayo, kwa sasa akili yetu tunailekeza kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, tunaenda Botswana tukiwa na lengo la ushindi," alisema Fadlu.

Aidha, alisema mashabiki waendelee kuiunga mkono timu hiyo kwakuwa mafanikio yanakuja mbele yao.

Wakati kocha wa Simba akisema hivyo, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu, amelalamikia maamuzi yaliyofanywa na waamuzi wa mchezo huo wa juzi.

Mangungu, alisema walikubaliana mechi zote za Simba na Yanga waamuzi wake watoke nje ya nchi kukwepa maamuzi ya hovyo lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hawajatimiza walichokubaliana.

"Tulikubaliana waamuzi watoke nje kwenye michezo hii ya Simba na Yanga, lakini tazama kilichotokea, waamuzi wamefanya yale yale tunayoyalalamikia," alisema Mangungu.

Mwenyekiti huyo pamoja na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo wamelalamikia goli pekee la Pacome Zouazoa kuwa halikuwa halali kwa kuwa kulikuwa na makosa.

Katika mchezo huo uliochezwa uwanja wa Benjamin Mkapa juzi, Yanga kwa mara nyingine waliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kutetea taji lao la Ngao ya Jamii.

Kufanyika kwa mchezo huo ni ishara ya kufunguliwa kwa msimu mpya wa Ligi Kuu wa 2025/2026 ambayo inaanza rasmi leo kwa michezo mbalimbali.