Folz ataka muda 'pira biriani'

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:10 AM Sep 30 2025
news
Picha Mtandao
Kocha Mkuu wa Yanga, Romain Folz.

WAKATI ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya leo kucheza dhidi ya Mbeya City, Kocha Mkuu wa Yanga, Romain Folz, amewataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa na subira kwani ana imani kikosi chake kitakuwa tishio na kucheza soka safi linalosubiriwa kwa hamu.

Akizungumza wakati wa maandalizi ya mchezo wa leo dhidi ya Mbeya City, kocha huyo amesema hana shida kabisa na wakosoajakini amewataka baada ya miezi michache waje kuzungumza tena wakati kikosi chake kitakapokuwa kimeimarika.

Kocha huyo amesema hayo kufuatia baadhi ya mashabiki wa Yanga, wachambuzi na baadhi ya wanahabari kudai licha ya kushinda lakini kikosi chake hakichezi kama kilivyozoeleka huko nyuma kwa makocha wengine waliopita.

"Sina shida kabisa na wakosoaji lakini baada ya miezi michache waje tena kuzungumza.

Naiandaa timu kufika mbali kwenye mashindano yote, nimekuwa nikifanya mabadiliko na najua sababu za kufanya hivyo, lakini pia najua napotaka timu ifike na nitaifikisha inapotakiwa, ni suala la muda tu," alisema kocha huyo.

Hata hivyo, Folz ndiye kocha mwenye takwimu nzuri zaidi za matokeo ya mwanzo wa msimu tofauti na makocha wengine waliopita, kama Nasredine Nabi, Miguel Gamondi na Sead Ramovic.

Folz, ameiongoza Yanga kushinda michezo sita, ikishinda mabao 13, ikiwa haijaruhusu bao lolote.

Alianza kuingoza Yanga ilipoifunga Rayon Sports ya Rwanda mabao 3-0, kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa, Rayon Days nchini Rwanda, ikaichapa Bandari ya Kenya bao 1-0 kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi, ikaidungua Simba bao 1-0, mchezo wa Ngao ya Jamii, kabla ya kuisasambua Wiliete de Benguela, ikiwa ugenini, mchezo wa mkondo wa kwanza, hatua za awali, Ligi ya Mabingwa Afrika, ikaitandika Pamba Jiji katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu, mabao 3-0, kabla ya kushinda mabao 2-0, mechi ya marudiano, hatua ya awali, Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumzia mchezo wa leo ambao utakuwa wa pili kwa Yanga ambao ni Mabingwa Watetezi, alisema utakuwa kama michezo mingine ingawa hautokuwa rahisi.

"Mechi hii ni kama zingine ambazo tumezicheza, hautokuwa mchezo rahisi, ila tumejindaa ili kushinda, utakuwa mchezo wa pili kwetu, ligi ni ndefu hivyo ni lazima nifanye mabadiliko, nawaomba tu watu watakaokuwa karibu waje kuangalia mechi hii," alisema kocha huyo.

Kocha wa Mbeya City, Malale Hamsini, alisema amewandaa kimbinu, kimwili na kiakili kukabiliana na timu ngumu ya Yanga.

"Maandalizi yamekamilika, tuna mchezo mgumu dhidi ya Yanga, tutashuhudia mchezo mzuri, wenye upinzani mkubwa na ufundi zaidi.

Hatuangalii Yanga imefanya nini katika mechi zilizopita kwa sababu hakucheza na Mbeya City, sisi pia tumejipanga kuikabili, lakini hata sisi tuko vizuri, hatukufungwa na Azam kwa sababu walikuwa wazuri kiufundi bali kwa mipira ya adhabu tu," alisema.

Aliongeza kuwa katika mchezo wa leo atachezesha mastraika wawili kwa sababu anachohitaji ni ushindi.

Katika michezo miwili iliyopita, Mbeya City imeshinda moja na sare moja, ikiwa ugenini iliichapa Fountain Gate bao 1-0, kabla ya kufungwa mabao 2-0, Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, dhidi ya Azam.