VITA ya kuendelea kuwania pointi katika mechi za Ligi Kuu Bara inatarajia kuendelea tena leo kwa Simba kuwakaribisha Namungo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa huku Azam FC ikiwafuata ‘Maafande’ wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Isamuhyo, Dar es Salaam.
Kuelekea mechi hiyo, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Selemani Matola, amesema suala la kupoteza nafasi nyingi zinazopatikana tayari amelifanyia kazi na kuwataka mashabiki watakaofika kuishangilia timu hiyo na wale watakaofuatilia kwenye televisheni watashuhudia mabadiliko makubwa.
Matola amesema katika michezo mwili iliyopita, mmoja wa Ligi ya Mabingwa Afrika na ule wa Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate, kikosi chake kilitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini wachezaji wake walishindwa kuzibadilisha kuwa magoli kitu ambacho ndiyo amekifanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi.
"Tulitengeneza nafasi nyingi katika michezo yetu iliyopita ya kimataifa, hata ule wa Fountain Gate hatukuzitumia, lakini tulirudi kwenye uwanja wa mazoezi, nadhani kesho (leo) tunaweza kuanza kuona mabadiliko, nafasi nyingi tutazitumia na kufanya kushinda ushindi mnono," alisema Matola.
Kocha huyo alisema mechi haitakuwa rahisi kutokana timu wanayokwenda kucheza nayo huwa inawasumbua kila wanapokutana.
"Haiwezi kuwa rahisi kwa sababu siku zote Namungo huwa wanatupa mechi ngumu sana, ina benchi zuri la ufundi, kwetu sisi tunachohitaji ni pointi tatu ili tuwe na pointi sita kwenye msimamo wa ligi.
Tutakwenda kwa tahadhari kubwa, tutawakosa Mohamed Bajaber na Abdulrazack Hamza ambao bado wanaendelea na majeruhi," alisema kocha huyo ambaye atasimama kwa mara ya kwanza kama kocha wa muda baada ya kuondoka kwa Fadlu Davids, aliyejiunga na Raja Casablanca ya Morocco.
Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, amesema wanajua ugumu wa mechi ya leo, lakini wamejiandaa kukabiliana nao.
"Tunakwenda kucheza na timu nzuri na wenye wachezaji wazuri, lakini tumejiandaa vizuri na tuko tayari kucheza nao, tunatarajiwa kuwapa Simba mechi ngumu, suala ya matokeo yatajulikana baada ya dakika 90," alisema Mgunda, ambaye pia amewahi kuifundisha Simba kama kocha wa muda.
Utakuwa ni mchezo wa pili wa Simba, ambayo iliifunga Fountain Gate mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza, huku ukiwa ni mchezo wa tatu kwa Namungo, iliyotoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Pamba Jiji katika mchezo wa kwanza nyumbani kabla ya kuifunga Prisons bao 1-0.
Wakati huo huo, baada ya kutinga raundi ya kwanza ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC leo itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kuwavaa JKT Tanzania katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Bara.
Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amesema wanakwenda kucheza na timu yenye nguvu, hivyo hauwezi kuwa kama mchezo wao uliopita dhidi ya Coastal Union ambao walipata ushindi wa mabao 2-1.
"Tuko nyumbani, lakini hakuna urahisi kwa sababu Coastal Union wanavyocheza ni tofauti na Azam wanavyocheza, tunakutana na timu bora yenye wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu, hatutawahofia ila tutawaheshimu.
Tunapaswa tu kuwa bora wakati hatuna mpira na wakati tukiwa na mpira na kama tukipata nafasi na tukazitumia basi tunaweza kushinda mechi," alisema Ahmad.
Mchezaji mwandamizi wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema wamejipanga vyema kukabiliana na JKT Tanzania na kuongeza mara nyingi zinapokutana timu hizo mbili mchezo unakuwa mgumu.
"Sisi kama wachezaji tumejiandaa vizuri, tunafuata maelekezo wa mwalimu, tunawajua JKT Tanzania wana timu nzuri sana, wana wachezaji wazuri waliowasajili msimu huu na watakuwa kwao na mara nyingi tukikutana panachimbika hasa," alisema Fei Toto.
Katika michezo kati ya timu hizo mbili msimu uliopita, zilitoka suluhu kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, kabla ya Azam kupata ushindi wa mabao 2-0, katika mchezo wa pili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED