Mbivu, mbichi KenGold, Pamba FC sasa Aprili 28

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:35 AM Apr 11 2024
 Jengo la ofisi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Picha: Maktaba
Jengo la ofisi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

TIMU mbili zitakazopanda daraja moja kwa moja kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao na zile zitakazokwenda kucheza mechi za mchujo zitajulikana rasmi Aprili 28, mwaka huu wakati wa Ligi ya Championship itakapofikia tamati.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inaonyesha zimebaki mechi tatu kwa kila timu ili kumaliza msimu huku timu mbili zinazotarajiwa kushuka daraja moja kwa moja, pia zitajulikana siku hiyo.

Hata hivyo, kutokana na msimamo ilivyo, huenda pia baadhi ya timu zitakazopanda Ligi Kuu Bara na kushuka zinaweza kuanza kujulikana baada ya michezo miwili ijayo.

KenGold inayoongoza katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 61, inahitaji pointi tano tu ili kufikisha pointi 66 ambazo zitafikiwa na Pamba FC pekee, hivyo inaweza kujihakikishia kupanda daraja endapo itakusanya pointi hizo.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, KenGold imebakisha mechi zake dhidi ya TMA kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha itachezwa Aprili 13, mwaka huu itakuwa nyumbani Aprili 21, Uwanja wa Sokoine, Mbeya dhidi ya FGA Talents na mechi ya mwisho Aprili 28, mwaka huu itamaliza dhidi ya  Polisi Tanzania kwenye uwanja huo huo.

Pamba iliyo nafasi ya pili ina pointi 58, imebakisha mechi zake dhidi ya FGA Talents (Uwanja wa Nyamagana, Mwanza), dhidi ya TMA (Uwanja wa Black Rhino, Arusha) na Aprili 21 dhidi ya majirani Mbuni FC kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha ambayo itafunga pazia.

Biashara United ambayo ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 56, itacheza nyumbani dhidi ya Green Warriors halafu itaenda ugenini kuivaa Pan African na baadaye kumalizana na Cosmopolitan, huku Mbeya Kwanza ikiwa nafasi ya nne kwa pointi 56 pia, ikiwa imebakisha mechi zake tarehe hizo hizo, dhidi ya Pan African, Green Warriors, na Transit Camp, zote ikichezea nyumbani, Nangwanda Sijaona.