Mwenge wa Uhuru watua Njombe, wito watolewa kuhifadhi mazingira

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 05:32 PM May 08 2025
Mwenge wa Uhuru watua Njombe, wito watolewa kuhifadhi mazingira
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenge wa Uhuru watua Njombe, wito watolewa kuhifadhi mazingira

Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, ametoa wito kwa Halmashauri ya Mji wa Njombe kuendelea na juhudi za kutunza na kuhifadhi mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ussi alitoa wito huo leo alipokuwa akikagua msitu wa Ilonganjaula, sambamba na kugawa mizinga 20 ya nyuki kwa kikundi cha Wahenga, wafugaji wa nyuki wanaohifadhi eneo hilo. Alipongeza juhudi za wananchi wa eneo hilo kwa kutovamia hifadhi hiyo, akieleza kuwa ni mfano wa kuigwa katika utunzaji wa mazingira.

"Naamini msitu huu utakuwa hazina kubwa kwa taifa. Hata watalii na wageni wanaweza kuvutiwa kutembelea hapa, hivyo kuwa kivutio kizuri kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika eneo hili," alisema Ussi.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Juma Sweda, alipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa na kueleza kuwa mwenge huo utembelea na kuzindua miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.5.