Tanzania imedhamiria kuongoza katika mageuzi ya kidigitali katika elimu barani Afrika ili kichocheo ukuaji wa uchumi, maendeleo ya kijamii na ushindani wa kimataifa, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 itafanikisha azma hiyo.
Kauli hiyo imetolewa Mei 8,2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, akifungua Kongamano la 18 la eLearning Afrika linalofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema ili kufanikisha azma hiyo nchi imeandaa mifumo kadhaa ikwemo Sera ya Taifa ya TEHAMA na Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali Tanzania 2024-2034.
Amesema wanaendelea kushirikiana na Serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wanazuoni ili kufanya eLearning kupatikana kwa gharama nafuu kwa kuzingatia makundi yote katika jamii.
“Mkakati wa Taifa wa Elimu ya Kidijitali na Programu ya Tanzania ya Kidijitali zinalenga kuimarisha miundombinu na huduma za kidijitali, uhakika wa teknolojia vifaa, muunganiko na rasilimali za eLearning kufika maeneo mbalimbali nchini pia nchi nyingine kutumia rasilimali zao katika kusaidia mageuzi ya kidijitali katika nchi zao,” amesema Dk. Biteko.
Amewahimiza wadau wa kongamano hilo kuwa ili mageuzi ya kidijitali ya Afrika yaweze kufanikiwa, lazima kuwezeshwa kwa nguvu kazi yenye ujuzi kuanzia umri mdogo.
Amesema Tanzania imefanya marekebisho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 na kuwa ni mfano muhimu, ikisisitiza uendelezaji wa ujuzi kuanza elimu ya msingi ikilenga kuhamasisha na kukuza matumizi ya teknolojia za kidijitali ili kukabiliana na upungufu wa walimu, kupanua upatikanaji wa elimu, na kuboresha ubora wa kujifunza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED