Tanzania yashiriki Mkutano wa Mazingira Duniani Denmark

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 05:37 PM May 08 2025
Tanzania kushiriki Mkutano wa Mazingira Duniani Denmark
Picha: Mpigapicha Wetu
Tanzania kushiriki Mkutano wa Mazingira Duniani Denmark

Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden umeratibu ushiriki wa ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Mazingira duniani, unaofanyika jijini Copenhagen, Denmark kuanzia jana na kuendelea leo.

Ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, ambapo zaidi ya mawaziri 30 wanaosimamia masuala ya mazingira kutoka nchi mbalimbali duniani, wakiwemo wawakilishi kutoka Kamisheni ya Umoja wa Ulaya na wadau wa kimataifa wa mazingira, wanashiriki mkutano huo.

Mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kupokea taarifa kutoka kila nchi kuhusu namna zinavyoshiriki katika kupunguza uzalishaji wa gesi joto duniani, kubadilishana uzoefu wa utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kuweka mipango ya maandalizi ya Mkutano wa COP 30 unaotarajiwa kufanyika Novemba 2025 nchini Brazil.

Tanzania imewasilisha ajenda mahsusi ikiwemo kuongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa programu za mabadiliko ya tabianchi, nishati safi ya kupikia, na kuhimiza utolewaji wa fedha zilizokuwa zimeahidiwa na wahisani mbalimbali kwa wakati unaofaa.

Vilevile, Tanzania imeshawishi wadau wa mazingira kutoa misaada yenye masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza programu za mazingira, kuwekeza katika teknolojia ya upimaji wa hewa ya kaboni, pamoja na kujenga uwezo wa kitaasisi kwa taasisi zinazoratibu masuala ya mazingira nchini.

Aidha, Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuendelea kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kupitia ubia wa kimkakati, sambamba na kutumia rasilimali za asili kama bahari, misitu, madini adimu, maziwa, mito na kujenga miundombinu rafiki kwa mazingira.