Mtanzania ashinda medali ya Dhahabu mashindano ya Dunia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:21 AM Sep 16 2025
news
Picha Mtandao
Mwanariadha Alphonce Simbu kulia akimaliza mbio katika mashindano ya riadha ya dunia.

MWANARIADHA Alphonce Simbu, ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mbio za riadha za Dunia za 2025 za kilometa 42.195.

Simbu alishinda medali hiyo katika mbio hizo zilizofanyika kwenye Uwanja wa Taifa wa Japan, jijini Tokyo jana, Jumatatu.

Simbu alimshinda kwa sekunde tatu tu, Amanal Petros raia wa Ujerumani na kuibuka mshindi wa kwanza akifanikiwa kushinda taji la dunia kwa kutumia muda wa saa 2:09:48.

Medali hiyo ya Dhahabu ya Dunia ya Simbu ni ya kwanza kwa mwanariadha wa Tanzania kuwahi kushinda.

“Nimeweka historia leo (jana), ni medali ya kwanza ya dhahabu ya Tanzania katika mashindano ya dunia,” alisema Simbu baada ya ushindi wake. 

“Nakumbuka mwaka 2017 kwenye mashindano ya Dunia ya London, nilishinda medali ya shaba na nilijiambia kwamba siwezi kukata tamaa, na hatimaye nimeweza kushinda medali ya dhahabu na kuweka historia.

“Nilikimbia mara nyingi, lakini sikupata medali yoyote, hivyo hatimaye nimeipata. Nilipofika hapa, nilijiambia kuwa sitakata tamaa. Nilibaki tu na kundi na ilinisaidia, na mashindano yalimalizika vizuri sana.”

Katika mbio hizo za kilometa 42.195 kwenye mazingira magumu, ziliamuliwa kwa utofauti mdogo sana.

Katika umaliziaji uliovutia wengi, Simbu alivuka mstari wa kumalizia mbele ya Mjerumani huyo kwa tofauti ya sekunde tatu.

RAIS SAMIA AMPONGEZA

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, jana alimpongeza Simbu kwa mafanikio hayo na heshima kubwa aliyoiletea nchi.

"Hongera sana Alphonce Simbu kwa Medali ya Dhahabu ya ushindi wa mbio ndefu za Mashindano ya Kimataifa ya Riadha ya Tokyo. Ndani ya saa 2:09:48 umeandika sehemu ya historia ya taifa letu. 

"Kama nilivyokusihi uliposhika nafasi ya pili kwenye Boston Marathon Aprili mwaka huu, ushindi wako ni matokeo ya nidhamu yako ya hali ya juu na kujituma kwa bidii kwenye kazi. Umekuwa mfano bora kuhusu nguzo hizo mbili za kazi kwa wanariadha na wanamichezo wenzako, na hata kwa wasio wanamichezo. Endelea kuipeperusha vema na kuiheshimisha bendera ya taifa letu," alisema Samia.

 

WENGINE NCHINI WALIOTISHA KIMATAIFA

Wakati Simbu yeye akiweka rekodi ya kushinda mashindano ya dunia, wapo pia wanariadha wengine nchini waliowahi kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa na kuiheshimisha Tanzania.

Suleiman Nyambui, ambaye alibobea katika fani mbalimbali za masafa marefu, alishinda medali ya shaba katika Michezo ya All-Africa ya 1978, medali ya fedha katika mita 5000 katika Olimpiki ya Majira ya 1980, na alimaliza wa kwanza katika mbio za marathon tatu mfululizo kati ya 1987 na 1988.

Pia Juma Ikangaa, ambaye alishinda rekodi kwenye mbio za New York City Marathon 1989 katika muda wa rekodi wa saa 2:08:01. 

Ikangaa pia alipendwa sana katika mbio za Boston Marathon baada ya kumaliza wa pili kwa miaka mitatu mfululizo kwenye Boston Marathon kuanzia 1988 hadi 1990.

Filbert Bayi pia alifanya vizuri mbio za kati ya miaka ya 1970. Aliweka rekodi za dunia za mita 1500 mwaka 1974 na maili mwaka 1975. Rekodi yake ya dunia katika mita 1500 pia ilikuwa rekodi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola hadi 2022.