NAHODHA wa Yanga, Bakari Mwamnyeto, amesema wanataka kuanza kwa kishindo mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu tanzania dhidi ya Pamba Jiji kama walivyofanya kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuichakaza Wiliete de Benguela ya Angola mabao 3-0.
Akizungumza kuelekea mchezo huo utakaopigwa kesho kutwa, Jumatano, Mwamnyeto alisema kama wameanza kwa kishindo kwenye ligi ya Mabingwa kwa kumpiga mtu mabao 3-0, basi wanataka kuendeleza kishindo kwenye Ligi Kuu dhidi ya Pamba, mchezo unaotarajiwa kupigwa, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
“Tumeambizana wachezaji wenyewe hakuna kulala, mechi msimu huu zitakuwa nyingi na hakutakuwa na muda mrefu wa kupumzika, nadhani inaweza kuwa kila baada ya siku tatu, mambo ni mengi lakini muda ni mchache,” alisema Mwamnyeto.
Alingeza; “Kwa maana hiyo tumetoka kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika tumeshinda mabao 3-0, sasa tunakwenda kucheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Pamba, tunataka kilichotokea kule Angola ndicho kitokee huku.”
Akizungumzia mchezo huo dhidi ya Wiliete, alisema baada ya ushindi wanajiandaa pia na mchezo wa marudiano utakaochezwa, Jumamosi ijayo, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
"Wachezaji wengi wa Yanga tumeshakuwa wazoefu kwenye michezo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, tuna utulivu wa mwili na akili, tumeanza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete, kwa sasa tunajiandaa na mchezo wa marudiano hapa nyumbani ili tuweze kupenya raundi ya kwanza,” alisema.
“Tunaamini kwa kazi tuliyoifanya kule Angola kinachotakiwa ni kuja kuimalizia tu hapa nchini ili tujue huko mbele tunaendaje," alisema.
Kikosi cha Yanga kiliwasili juzi kutoka nchini Angola, ambapo kwa sasa kinajiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu.
Yanga imekuwa ni moja kati ya timu nne za Tanzania zilizopata ushindi ugenini kwenye michuano ya kimataifa wikiendi hii.
Mabingwa hao Watetezi wa Ligi Kuu, wakiwa Uwanja wa 11 Novembro, Luanda, waliwafunga wenyeji wao, Wiliete mabao 3-0, yakiwekwa ndani ya wavu na Aziz Andabwile, Edmund John na Prince Dube.
Baada ya Yanga kuonesha njia Ijumaa, kesho yake, Simba nayo ikiwa Uwanja
Obed Itani Chilume iliifunga Gaborone United bao 1-0 lililowekwa wavuni na Elie Mpanzu, ukiwa pia ni mchezo wa mkondo wa kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika hatua za awali.
Jumamosi hiyo hiyo, wawakilishi wengine wa nchi kwenye michuano ya kimataifa, Azam FC ilipata ushindi mabao 2-0 ikiwa ugenini, Sudan Kusini, kwenye uwanja wa Juba, ikicheza dhidi ya Al Mereikh Bentiu, wakati nchini Rwanda, Singida Black Stars nayo ikipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rayon Sports, Uwanja wa Nyamirambo, Kigali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED