MACHO na masikio ya mashabiki wa soka nchini, leo yataelekezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakati watani wa jadi kwenye mpira wa Tanzania, Simba na Yanga watakapopambana kuanzia saa 11:00 jioni, kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu 2025/26.
Utakuwa ni mchezo wa 11 kwa timu hiyo kukutana kwenye Ngao ya Jamii, huku ukiwa ni wa 21, tangu kuanza kwa mechi hizo, zamani likiitwa Kombe la Nyerere, 2001.
Timu yoyote itakayoshinda leo itakuwa imefanya hivyo mara sita na kujiwekea rekodi ya kushinda mara nyingi zaidi, kwa kuizidi nyingine mara moja, kwani zilipokutana katika michezo 10 iliyopita, kila timu ilishinda mara tano.
Mabingwa Watetezi, Yanga, waliifunga Simba mabao 2-1, 2001, mabao 3-1 kwa mikwaju ya penalti 2010, bao 1-0, 2021, mabao 2-1, 2022 na bao 1-0, mwaka jana.
Simba ilishinda mechi zake za Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, 2002, mabao 4-1, mabao 2-0, 2005, mwaka 2011, ilishinda tena mabao 2-0, ikashinda kwa mikwaju ya penalti 5-4, 2017, kabla ya kushinda tena kwa mikwaju ya penalti 3-1, 2023, mechi pekee iliyochezwa nje ya Dar es Salaam, Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Yanga inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuifunga Simba bao 1-0 mwaka jana, Agosti 8, lililowekwa wavuni na Maxi Nzengeli.
Kama vile haitoshi, Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi nzuri ya kuifunga Simba mara tano mfululizo katika mashindano tofauti.
Mara ya mwisho iliifunga Simba mabao 2-0, katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, uliochezwa Juni 25, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kabla ya hapo, ilishinda mabao 5-1, mechi ya mzunguko wa kwanza Ligi Kuu msimu wa 2023/24, Novemba 5, 2023, ikishinda tena mabao 2-1, mechi ya mzunguko wa pili msimu huo, Aprili 20, 2024.
Yanga ilidungua tena Simba, bao 1-0, Agosti 8, mwaka jana, katika mchezo wa Ngao ya Jamii, kabla ya kupata ushindi wa bao 1-0 kwa mara nyingine, Oktoba 19, mwaka jana, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
Kocha Mkuu wa timu ya Simba, Fadlu Davids, amesema kuwa Yanga ndio wana presha ya mchezo huo kwa kuwa wana benchi jipya la ufundi.
"Kwa upande wangu sina presha na mchezo huo, Yanga ndiyo wenye presha kwa sababu wana benchi jipya la ufundi," alisema Davids
Aidha, alisema maandalizi kuelekea kwenye mchezo huo yanaendelea vizuri na kuweka wazi atamkosa mchezaji wake Mohamed Bajabir ambaye ni majeruhi.
Hata hivyo, alisema kiungo wake mkabaji aliyesajiliwa msimu huu kutokea Coastal Union, Hussein Semfuko, anaendelea vema na huenda akawepo kwenye mchezo wa leo, ingawa anasubiri majibu ya mwisho ya daktari kwani pia alikuwa majeruhi.
Alisema licha ya kuwa na wachezaji wengi wapya, atapambana ili apate ushindi na kufuta ule uteja wa kufungwa na wapinzani wake.
Fadlu alisema anaupa umuhimu mkubwa mchezo huo kwa kuwa anatambua ni miongoni mwa mchezo mkubwa wenye ushindani kutokana na aina ya timu wanayokutana nayo.
Aliongeza kuwa makosa yaliyofanywa na wachezaji wake msimu uliopita, anaendelea kuyafanyia kazi ambapo anaamini ongezeko la wachezaji wapya litaleta mabadiliko.
Shomari Kapombe ambaye alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, alisema wapo tayari kwa ajili ya kukutana na mpinzani wao huyo, lakini wataingia kwa tahadhari kwa kuwa anatambua Yanga msimu uliopita safu yao ya ushambuliaji ilikuwa hatari, lakini kwa sasa wameimarisha safu yao ya ulinzi.
"Tutaingia kwa tahadhari katika mchezo huo naamini safu yetu ya ulinzi kwa sasa ipo imara kutokana na maingizo mapya, makosa tuliyoyafanya msimu uliopita, tutayafanyia kazi yasijirudie kwenye mchezo wetu," alisema
Pia, alisema wamekaa na wachezaji wapya na kuwaeleza ugumu na umuhimu wa mchezo pamoja na kuwapa mbinu zitakazowafanya wafanye vizuri.
Kocha Mkuu wa Yanga, Romain Folz, alisema mchezo utakuwa mgumu na ushindani, lakini amejiandaa vema na anawaamini wachezaji wake kuwa watafanya kile alichowaelekeza.
"Kwa upande wangu nimejiandaa vizuri kwa mchezo huo, najua ni mgumu ambao utakuwa na ushindani mkubwa, nawaamini wachezaji wangu wana uzoefu na mechi hizi kubwa, watafanya nilichowaelekeza. Nina majeruhi mmoja tu ambaye sitomtaja hapa," alisema.
Dickson Job, nahodha msaidizi wa Yanga, amesema wapo tayari kwa mchezo huo na watafuata yote waliyoelekezwa na benchi la ufundi.
"Huu ni mchezo muhimu, sisi kama wachezaji tupo tayari, tumeona jinsi Simba walivyocheza kwenye mchezo wao wa kirafiki wa kimataifa, siku ya Kilele cha Simba Day, hivyo tunajua sehemu ya kuwabana," alisema Job.
Msemaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Cliford Ndimbo alisema mwamuzi wa kati katika mchezo huo atakuwa ni, Ahmed Arajiga, akisaidiwa na Mohamed Mkono pamoja na Kassim Mpanga, huku wa akiba akiwa ni Ramadhan Kayoko wakati mwamuzi wa tathimini akimtaja kuwa ni Soud Abdi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED