Simba Day kutikisa nchi leo

By Adam Fungamwango ,, Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 12:26 PM Sep 10 2025
news
Picha Mtandao
Mashabiki wa Klabu ya Simba wakishangilia timu yao.

WAASISI wa matamasha Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Simba, leo wanatarajiwa kutikisa nchi, watakapofanya tamasha lao la 17 maarufu 'Simba Day', kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuanzia asubuhi hadi jioni, watakapokamilisha kwa mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.

Huu ni mwendelezo wa kila mwaka, tangu 2009, lilipoanzishwa kwa mara ya kwanza chini ya Mwenyekiti, Hassan Dalali, ambapo hufanya kilele cha tamasha kwa burudani mbalimbali uwanjani kutoka kwa wasanii mbalimbali walioteuliwa, mechi za utangulizi na baadaye kufuata ule wakati ambao wanachama, mashabiki wengi wanaupenda kabla ya kuanza kwa mchezo, nao ni kutangazwa kwa wachezaji wa zamani na wapya watakaounda kikosi cha msimu.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema huu ni wakati mzuri wa wanachama na mashabiki kuona kikosi chao kipya, akiongeza kuwa msimu uliopita walijenga msingi wa kikosi hicho, lakini msimu huu sasa wanajenga ukuta.

"Maandalizi yamekwenda vizuri, tulikuwa na wiki sita za 'pre season', kikosi changu kimekamilika kwa mchezo wa Simba Day na Ngao ya Jamii.

"Ni wakati wa wanachama na mashabiki kuja kuangalia kikosi chao kipya, ni kikosi kitakachokuwa na mabadiliko makubwa kutokana na usajili uliofanyika, wachezaji wengi wapya na wenye uzoefu wamesajiliwa.

"Kuna baadhi wameondoka, lakini tumepata mbadala wao, msimu uliopita tulianza na msingi, sasa tunajenga ukuta. 

"Malengo yangu ni kuona tunapata makombe mengi msimu ujao kwa kushinda michezo yetu tunataka turudishe heshima yetu Simba," alisema kocha huyo. 

Mohamed Bajaber ambaye alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, alisema yupo tayari kwa ajili ya mchezo huo. 

"Kwa upande wetu tupo tayari kwa ajili ya mchezo wetu huo, tunafahamu tunakutana na timu nzuri na sisi tupo vizuri kwani tumefanya maandalizi ya kutosha," alisema Bajabir. 

Itakuwa ni Simba Day ya pili kwa mwalimu Fadlu ambaye alichukua mikoba ya kuifundisha timu hiyo msimu uliopita.

Kocha Mkuu wa Gor Mahia, Charles Akonnor, yeye amesema wanakwenda kucheza mechi ngumu dhidi ya timu kubwa Afrika, lakini wamejipanga kushinda mchezo huo ili kujiweka vema kwa ajili ya Ligi Kuu ya Kenya inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

"Tunaona fahari kuwa hapa, tunaona fahari kupata nafasi ya kuja kushuhudia na kucheza soka kwenye tamasha hili, hata sisi Kenya tunaijua Simba Day, pia tunaifahamu klabu ya Simba kuwa ni moja ya vikosi vikubwa na bora barani Afrika.

"Pamoja na hayo sisi tumekuja kushindana, sisi pia tunakiandaa kikosi chetu kwa msimu mpya wa mashindano na kuangalia ni namna gani tutakwenda kuanza ligi. Mechi hii kubwa dhidi ya Simba itatupa kipimo halisi kabla ya kuanza Ligi Kuu ya Kenya kwa maana hiyo tumejiandaa kushinda mechi hii, ila tunaamini utakuwa mchezo mkubwa na mgumu," alisema Akonnor.

Felimon Otieno, ambaye alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake wa Gor Mahia, alisema wapo vizuri kukutana na Simba licha ya kuwa ni timu kubwa barani Afrika. 

"Tunatambua Simba ni timu kubwa, tutapambana ili kuwapa burudani mashabiki wetu waliopo hapa nchini," alisema Otieno. 

Baadhi ya wachezaji wapya waliosajiliwa na Simba ambao wataonekana kwa mara ya kwanza leo ni Selemani Mwalimu, akitokea Wydad Casablanca ya Morocco, Wilson Nangu na Yakoub Suleiman, waliosajiliwa kutoka JKT Tanzania, Jonathan Sowah, raia wa Ghana, aliyesajiliwa kutoka Singida Black Stars.

Wengine ni Mkenya, Mohamed Bajaber kutoka Polisi ya Kenya, Rushine De Reuck na Neo Maema, wote raia wa Afrika Kusini kutoka Mamelodi Sundowns ya nchini humo, Antony Mligo akitokea Namungo FC, Mourice Abraham kutoka RFK Novi Sad ya Serbia na Allasane Kante, raia wa Senagal, aliyesajiliwa kutoka CA Bizertin ya Tunisia na Naby Camara raia wa Guinea, akitokea Al Waab FC ya nchini Qatar.

Simba ilicheza tamasha la kwanza mwaka 2009, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam chini ya Kocha Mzambia, Patrick Phiri, ikishinda bao 1-0 dhidi ya SC Villa ya Uganda, lililofungwa na mchezaji ambaye aliichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza, Hilary Echessa, raia wa Kenya. Mbali na kiungo huyo, wachezaji wapya walioatambuliwa siku hiyo ni Joseph Owino aliyesajiliwa kutoka URA ya Uganda na Emmanuel Okwi, akitokea timu hiyo waliocheza nayo, wote wakiwa raia wa Uganda.

Baada ya hapo klabu nyingi Ukanda wa CECAFA ikiwamo za hapa nchini nazo zikaanza kufanya matamasha yao kwa mfumo na mtindo ule ule wa Simba.

Msimu uliopita, Simba ilicheza Simba Day ya 16 dhidi ya APR ya Rwanda na kushinda mabao 2-0, Agosti 3, mwaka jana, kwa mabao ya Debora Fernandes Mavambo na Edwin Balua, wote wakiwa wachezaji wapya, lakini hawatokuwapo kwenye kikosi cha leo kwani wameshaondoka kwenda kuzichezea klabu zingine.