Simba Day yageuka kuwa zaidi ya mtoko

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:28 AM Sep 11 2025
news
Picha Mtandao
Mashabiki wa klabu ya Simba wakifurahia wakati wa sherehe za Simba Day jana, Dar es Salaam.

HAIJAWAHI kutokea! Ndicho unachoweza kusema unapotaka kusimulia Tamasha la Simba Day, mahususi kwa ajili ya kutambulisha wachezaji wao wa msimu mpya wa 2025/26, ambalo lilifanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana.

Tamasha hilo, ambalo Simba imekuwa ikilifanya kila mwaka kabla ya kuanza msimu mpya, lilipambwa na wasanii mbalimbali pamoja wakitoa burudani ambazo zilikongo nyoyo za mashabiki waliohudhuria uwanjani hapo.

Katika tamasha hilo la 17 kwa Simba kulifanya, mbali na wageni mbalimbali maarufu waliohudhuria, waliongozwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ambaye alikuwa mgeni rasmi huku likihitimishwa na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.

HALI YA UWANJA

Wanachama na mashabiki wa timu hiyo walijitokeza kwa wingi, wakiujaza uwanja mapema kwa ajili ya kupata burudani toka kwa wasanii mbalimbali.

Mbali na viongozi wa serikali, viongozi wa Simba, wakiongozwa na Mwwenyekiti wa mpya wa Bodi ya Wakurugenzi, Crecentius Magori, mjumbe mpya, Barbara Gonzalez, alikuwapo pia Mwekezaji na Rais wa Heshima wa Klabu hiyo, Mohamed 'Mo' Dewji.

WASANII

Wasanii waliovutia na kuwatia wazimu mashabiki uwanjani hapo ni Chino Wanaman, ambaye aliburudisha kwa ngoma zake kadhaa, lakini zilizowachengua uwanjani hapo ni 'Yesa' maarufu kama 'Funga Mageti,' pamoja na 'Gibela remix', ambazo ziliwafanya waliokaa kwenye viti kunyanyuka na kuanza kucheza huku nao wakiimba pamoja naye.

MBOSO

Shughuli pevu ilikuwa kwa msanii Mbosso, ambaye alipanda kwa mbwembwe na kuburudisha kwa nyimbo zake nyingi za kuchezesha na za taratibu zilizopokelewa kwa bashasha na mashabiki waliokuwa wanakwenda naye sambamba kwa kuimba na kucheza.

Ngoma zilizotia fora ni 'Selemani', 'Athumani', na 'Pawa'.

Dj Sinyorita 

Mwanadada, Dj Sinyorita naye hakuwa nyuma kuwarusha mashabiki waliofurika uwanjani hapo kwa ngoma mbalimbali wakicheza na kufurahi bila kujali joto na jua kali.

Awali, bendi ya African Stars ikitumia mtindo maarufu wa 'Twanga Pepeta', chini ya uongozi wake mwanamuziki mkongwe Luiza Mbutu, iliifanya balaa kubwa uwanjani, ikiwa na wachezaji shoo wake ambao walionesha umahiri mkubwa wa kucheza sebene lililopewa jina, 'We Huigopi?'

UTAMBULISHO WA WACHEZAJI

Baada ya burudani zote lilifuata tukio muhimu la siku la utambulisho wa wachezaji wa msimu mpya ambapo, Meneja Habari wa Klabu hiyo, Ahmed Ally alikaribishwa jukwaani na kuanza kulitambulisha benchi la ufundi kabla ya kutambulisha nyota wa kikosi hicho kwa msimu wa 2025/26.

NYOTA WAPYA

Miongoni mwa wachezaji watakaounda kikosi cha msimu wa 2025/26, Simba imewatangaza wachezaji wapya 13 watakaokiongozea nguvu, sita wakiwa wakigeni na saba wachezaji wazawa.

Wachezaji saba wazawa ni Selemani Mwalimu, akitokea Wydad Casablanca ya Morocco, Wilson Nangu na Yakoub Suleiman ambao wote walisajiliwa kutoka JKT Tanzania.

Wengine ni Mourice Abraham kutoka, RFK Novi Sad ya Serbia, Antony Mligo kutoka Namungo, Vedastus Masinde aliyesajiliwa kutoka TMA inayocheza Ligi ya Championship, na Charles Daud Semfuko akitokea Coastal Union.

WAKIMATAIFA

Wachezaji kutoka nje ya nchi ni Jonathan Sowah, raia wa Ghana, aliyesajiliwa kutoka Singida Black Stars, Mkenya, Mohamed Bajaber kutoka Polisi ya Kenya, Rushine De Reuck na Neo Maema, wote raia wa Afrika Kusini kutoka Mamelodi Sundowns ya nchini humo, Allasane Kante, raia wa Senagal, aliyesajiliwa kutoka CA Bizertin ya Tunisia na Naby Camara, raia wa Guinea, akitokea Al Waab FC ya nchini Qatar.

WACHEZAJI WALIOBAKI

Wachezaji waliobaki kwenye kikosi cha Simba kuelekea msimu ujao ni 12, nao ni Moussa Camara, Hussein Abel, Shomari Kapombe, Karaboue Chamou, Yusuph Kagoma, Elie Mpanzu, Jean Charles Ahoua, Steven Mukwala, Joshua Mutale, Mzamiru Yassin, Kibu Denis na Ladack Chasambi.

WALIOONDOKA

Msimu ujao haitakuwa na wachezaji waliotumika msimu uliopita ambao ni Edwin Balua, Debora Mavambo, Fondoh Che Malone na Leonel Ateba ambao wameondoka na kusajiliwa na klabu mbalimbali nje ya nchi.

Wengine ni Velentino Mashaka na Salehe Karabaka ambao wamepelekwa JKT Tanzania kwa mkopo.