KLABU ya Simba imesema imebakisha jina la mchezaji mmoja tu ili kufunge zoezi la kutambulisha wachezaji wapya kuelekea msimu ujao wa mashindano, huku ikisema bado haijamuuza straika wao, Steven Mukwala kama inavyodaiwa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema limebaki jina la mchezaji mmoja tu ili kufunga zoezi hilo, akiahidi huenda lingeweza kutangazwa jana au leo kwenye vyanzo rasmi vya klabu.
"Kuhusu usajili imebaki jina moja, tuna mchezaji mmoja bado hatujamtambulisha, ngoja niingie ofisini niangalie utaratibu unasemaje, kama kila kitu kitakuwa tayari basi leo (jana), au kesho (leo), tunaweza kutangaza na ndiye atakuwa mchezaji anayefunga dimba kwa kutangazwa msimu huu, kabla ya Simba Day, hapo kesho," alisema Ahmed.
Alisema wamechelewa kulitangaza kutokana na kuwa kwenye harakati za kumalizia taratibu zote zinazotakiwa ili waweze kuliweka hadharani.
Baadhi ya wachezaji wa Simba waliosajiliwa na kutangazwa mpaka sasa ni Selemani Mwalimu, akitokea Wydad Casablanca ya Morocco, Wilson Nangu na Yakoub Suleiman, waliosajiliwa kutoka JKT Tanzania, Jonathan Sowah, raia wa Ghana, aliyesajiliwa kutoka Singida Black Stars, Mkenya Mohamed Bajaber kutoka Polisi ya Kenya, Rushine De Reuck na Neo Maema, wote raia wa Afrika Kusini kutoka Mamelodi Sundowns ya nchini humo.
Wengine ni Antony Mligo akitokea Namungo FC, Mourice Abraham kutoka, RFK Novi Sad ya Serbia na Allasane Kante, raia wa Senagal, aliyesajiliwa kutoka CA Bizertin ya Tunisia na Naby Camara, raia wa Guinea, akitokea Al Waab FC ya nchini Qatar.
Wakati hayo yakiendelea, Ahmed, amesema mpaka sasa straika Mukwala bado ni mchezaji wa Simba na hajauzwa kwenye klabu yoyote mpaka sasa.
Alisema kuwa hata yeye amezisoma taarifa hizo kutoka vyanzo mbalimbali vya habari, lakini mpaka jana hakuna taarifa yoyote rasmi ya mauziano ya Simba na Klabu ya Al Ittihad ya Libya kumtaka mchezaji huyo.
"Mukwala ni mchezaji wa Simba, bado ana mkataba na Klabu ya Simba, ana mwaka mmoja zaidi wa kuitumikia, zipo taarifa niliziona wikiendi hii za klabu ya moja ya Libya, Al Ittihad, lakini hadi naamka leo hii (jana), biashara hiyo haijafanyika, naamini itabaki hivyo," alisema Ahmed.
Alisema kutokana na muda wa usajili kuwa si rafiki, hawawezi kufanya biashara hiyo kwani wasingeweza kupata mchezaji wa kuweza kuziba pengo lake kwa sasa.
Taarifa zinasema kuwa klabu ya Al Ittihad ya Libya imekubali kutoa kiasi cha Sh, bilioni 2.4 za Kitanzania ili kumsajili straika wa huyo wa Simba raia wa Uganda, Mukwala.
Habari kutoka vyanzo mbalimbali vya habari Afrika, zinasema klabu hiyo imeandaa mkataba wa miaka miwili huku maslahi binafsi kati ya pande mbili za mchezaji na klabu zikiwa zimekubaliwa.
Hata hivyo, kilichokuwa kikisubiriwa ni klabu ya Simba kukubali ofa hiyo, ambapo yenyewe ndiyo itaamua kama impige bei au la.
Juzi saa sita usiku ilikuwa siku ya mwisho ya usajili na uhamisho wa Klabu za Ligi Kuu, Championship, 'First League', na Ligi ya soka Wanawake.
Kwa maana hiyo, iwapo Simba ikimuuza Mukwala, haitapata nafasi ya kusajili mchezaji mwingine wa kuchukua nafasi yake kwa sasa mpaka kipindi cha dirisha dogo la usajili, Januari mwakani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED