Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC, Seleman Matola, amesema kikosi chake kipo tayari kuvaana na Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Simba inashuka uwanjani ikiwa na morali ya juu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3–0 dhidi ya Fountain Gate kwenye mchezo uliopita, sambamba na kupenya hatua ya pili ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Matola amesema maandalizi yamekamilika na kikosi chake kipo tayari kwa ushindi.
"Haitakuwa mechi rahisi kutokana na aina ya benchi la ufundi la Namungo, lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata pointi tatu," amesema Matola.
Ameongeza kuwa kikosi chake kimeanza mazoezi mara tu baada ya mchezo wa marudiano dhidi ya Gaborone United, akisisitiza anaendelea kuboresha safu ya umaliziaji ili kuhakikisha nafasi zinazopatikana zinatumika vyema.
Hata hivyo, Matola amesema kikosi chake kitawakosa wachezaji wawili waliopo majeruhi wa muda mrefu, Mohamed Bajaber na Abdul Razack, huku wengine wakiwa katika hali nzuri ya mchezo.
Kwa upande wake, mchezaji Antony Mligo, akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, amesema kikosi kimejipanga kuhakikisha kinaendeleza ushindani.
"Kwa upande wetu wachezaji tumejipanga vizuri kuhakikisha tunaendeleza ushindani katika mchezo huu ambao tunatarajia utakuwa mgumu," amesema Mligo.
Kocha Mkuu wa Namungo FC, Juma Mgunda, amesema nao wako tayari kwa pambano hilo, akitambua ugumu wa kukutana na Simba.
"Tupo tayari kukabiliana na Simba. Tunafahamu hivi karibuni wametoka kwenye mchezo wa kimataifa, lakini tutapambana ili kuwapatie mashabiki wetu burudani," amesema Mgunda.
Naye mchezaji Abdala Mfuko, kwa niaba ya wenzake, amesema wapo tayari kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya katika mchezo huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED