Simba, Tabora Utd zatunishiana misuli

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:05 AM Jan 24 2025
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally
Picha: Mtandao
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally

SIMBA ya jijini, Dar es Salaam imewaonya Tabora United haiwezi kuwazuia kupata ushindi katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa Februari 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani, Tabora.

Wekundu wa Msimbazi wametamba kamwe Tabora United haitaweza kufanya kile ilichowafanyia Yanga na Azam FC na kuwataka wajiandae 'kuteseka' katika mchezo huo.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema jana, amezisikia tambo za Tabora United  wameangusha vigogo vyote na aliyebaki ni Simba tu, hivyo kuwatahadharisha msimu huu wamedhamiria kupata ushindi kwenye uwanja wowote na kwa timu yoyote wanayokutana nayo.

"Wana haki ya kutamba, wamefanya mambo makubwa, wamechukua pointi tatu dhidi ya Yanga na Azam FC, si jambo dogo, wana haki ya kujivunia, lakini wasitufananishe na watu wengine, kama mzunguko wa kwanza wanasema tuliwakuta hawajakaa vizuri, basi wajue hata Februari 2, tukiwafunga watasema tena hawajakaa vizuri.

Sisi msimu huu tumedhamiria kufanya vyema na tunataka kushinda kila mchezo, tunawaheshimu wana timu ngumu, wana morali ya kutosha, lakini siyo timu ya kutuzuia sisi," Ahmed alisema.

Ahmed alisema kikosi cha Simba kilitarajia kurejea kambini leo baada ya mapumziko waliyopewa kufuatia kumaliza kibarua cha michezo ya hatua ya makundi ya michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya CS Constantine na kuongoza Kundi A.

"Tunarejea uwanjani kesho tarehe 24 (leo), kwa sababu tarehe 26 (Jumapili) tuna mchezo dhidi ya Kilimanjaro Wonders, tangu walipocheza dhidi ya CS Constantine vijana walipewa mapumziko, baada ya mchezo huo kambi haitavunjwa, itaendelea kwa ajili ya mchezo wa Februari 2 dhidi ya Tabora United," Ahmed alisema.

Ofisa Habari wa Tabora United, Christina Mwagala, ameendelea kutamba sasa wanamsubiri kumfunga Simba kama walivyotembeza kichapo walipokutana na Yanga na Azam.

Mwagala alisema Simba inatakiwa ijiandae kupita katika njia ambayo 'wenzake' wamepita msimu huu walipokutana nao.

Tabora United ambayo haikuanza vyema msimu chini ya Kocha Mkenya, Francis Kimanzi, ambaye alitimuliwa lakini iligeuka ghafla na tishio ilipomtwaa Mkongomani, Anicet Kiazmak, aliyebadilisha kwa kiasi kikubwa na kuanza kutoa vichapo vya kushangaza.

Novemba 7, mwaka jana ilitoa kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Yanga mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex huku Desemba 13, ikiwaadhibu Azam FC, mabao 2-1.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Agosti 18, mwaka jana Tabora United ilichapwa mabao 3-0 na Simba, lakini ikidai matokeo hayo yalisababishwa na baadhi ya wachezaji wake wa kigeni kukosa vibali vya kucheza soka hapa nchini.

Hata hivyo, kabla ya mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba itakutana na Kilimanjaro Wonders katika mchezo wa raundi ya tatu ya mashindano ya Kombe la FA utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Ligi Kuu Tanzania Bara imerejea tena mapema baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kutangaza kusogeza mbele Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), ambayo awali ilitarajia kufanyika kuanzia Februari Mosi, mwaka huu.