TUTAANZA kwa kishindo, hayo ni maneno ya Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, kuelekea mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Fountain Gate itakayochezwa leo kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Matola alisema wanataka kuanza msimu mpya kwa kishindo kwa sababu msimu huu wamedhamiria kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na si jambo lingine.
Matola alisema si tu wanahitaji kupata ushindi katika mchezo wa leo, bali kuvuna ushindi wa kishindo.
"Lengo letu ni kupata pointi tatu na ushindi wa kwanza kwenye Ligi Kuu ingawa tunajua haitakuwa mechi rahisi, Fountain Gate walipoteza mchezo uliopita, hawatataka kupoteza tena mchezo wa pili, ila sisi tunataka kuanza msimu kwa kishindo, lengo letu msimu huu ni kuchukua ubingwa, kwa maana hiyo ni lazima tuanze na pointi tatu kwanza," alisema Matola.
Kocha huyo alisema ana uhakika wa kuondoka na furaha kwa sababu mchezo huo utachezwa kwenye uwanja (Benjamin Mkapa), waliouzoea ambao pia wana bahati nao.
"Tumefurahia sana kwenda kucheza kwa Mkapa, ni uwanja ambao huwa siku zote tukicheza tunafanya vizuri," Matola, kiungo na nahodha wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi alisema.
Aliongeza kikosi chote kiko kamili na wachezaji wote wapo kambini, isipokuwa Mohamed Bajaber, ambaye bado ni majeruhi.
Kuhusu mabadiliko ya kocha, ambapo kwa sasa wataongozwa na Kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Hemed Suleiman 'Morocco' baada ya Fadlu Davids kuondoka, alisema ni mabadiliko ya kawaida ambayo hayajawatoa wachezaji mchezoni.
"Wachezaji wa Simba ni wachezaji wa kimataifa, wanajua kabisa haya mambo huwa yanatokea na hayawezi kuwaondoa kwenye mchezo, au kuwafanya waathirike kisaikolojia, kwa hiyo sisi wote akili yetu ni mchezo huu tu," aliongeza Matola.
Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Denis Kitambi, amesema bado changamoto za kuwa na wachezaji wachache katika kikosi chake zinaendelea.
Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Kitambi amebainisha kuwa wamejiandaa kucheza dhidi ya Simba kwenye mazingira magumu.
"Maandalizi yetu kuelekea kwenye mchezo wa Simba ni magumu, nadhani taarifa mtakuwa nayo changamoto ambayo tunapitia kuhusiana na idadi ya wachezaji wetu ambao wameruhusiwa kutumika kwa ajili ya mchezo wa kesho (leo).
Ukiondoa hilo tumefanya mazoezi mazuri, tupo na wachezaji ambao watatumika na wale ambao bado hawawezi kutumika kwenye mchezo huo," alisema Kitambi
Siku chache zilizopita, uongozi wa klabu hiyo uliandika barua kwa Bodi ya Ligi kuomba mchezo huo usogezwe mbele kutokana na kuwa na idadi ndogo ya wachezaji waliothibitishwa kucheza mpaka sasa, lakini imeshindikana.
Pamoja na hayo, amesema amesema wapo tayari kuikabili Simba licha ya matatizo yote hayo.
"Tumewaona Simba wanavyocheza katika michezo yao mitatu ya Simba Day, Ngao ya Jamii na ule wa Ligi ya Mabingwa, lakini sisi tumejikita zaidi kutatua mapungufu yetu tuliyoyaona katika mchezo dhidi ya Mbeya City ambao tulipoteza kwa bao 1-0.
Mpinzani tunayecheza naye ni Simba, sidhani kama atatupa nafasi nyingi kama tulivyopata dhidi ya Mbeya City, kwa maana hiyo chache zinazopatikana inabidi tuzitumie," Kitambi alisema.
Katika mchezo dhidi ya Mbeya City uliochezwa Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Fountain Gate ilishuka dimbani ikiwa na wachezaji wachache na hiyo inatokana na kile ambacho klabu hiyo imekieleza tatizo la kiufundi katika mfumo wa usajili wa kimataifa (TMS).
Taarifa zinasema huenda Fountaine Gate wakachezesha wachezaji wasiotimia 11 katika mchezo wa leo. Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea tena keshokutwa kwa Maafande wa Prisons kuwakaribisha KMC wakati Coastal Union ya Tanga itawafuata Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED