WACHEZAJI wa Simba wameahidiwa kiasi cha Sh. Milioni 100, iwapo wataifunga Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, unaotarajiwa kucheza kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni ishara ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2025/26.
Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ambayo ni moja ya wadhamini wa klabu hiyo, Joseph Rwegasira, alipozungumza majukumu yao kuelekea kwenye mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka nchini.
Mbali na kiasi hicho, Rwegasira pia ameahidi kuwa kampuni yake itatoa kiasi cha Sh. Milioni 10, kwa golikipa yeyote atakayesimama langoni na kumaliza dakika 90 bila kuruhusu bao.
"Tunajivunia kuingia kwenye dabi ya kwanza tangu tuanze kuidhamini klabu hii, tuna imani kuwa timu yetu itaenda kufanya vizuri, nimeiona timu yetu kwenye tamasha la Simba Day, nimewaangalia na watani zetu, kuna kila sababu ya Simba kwenda kufanya vizuri,” alisema.
“Na sisi tunadhani ili wafanye vizuri, tumeona tuahidi jambo kwamba ikishinda huo mchezo dhidi ya Yanga, tutatoa Sh. Milioni 100 kwa ajili ya wachezaji ambao wataiwezesha timu kupata ushindi, kwa sababu ni muhimu na tunauhitaji sana," alisema Mkurugenzi huyo.
“Yoyote kati ya makipa wawili, Moussa Camara au Yakoub Suleiman, ataondoka na Sh Milioni 10, iwapo atapata 'clean sheet' kwenye mchezo huo.
“Nia yetu ni kwa ajili ya kuwatia hamasa wachezaji, najua hata klabu nayo ina utaratibu wake, nako pia kuna bonasi zao ambazo watatoa, ila sisi kwa sababu tumeingia makubaliano na klabu tunapaswa na sisi tujitolee," alisema.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameitaja mechi hiyo kuwa ni ya kutengeneza heshima.
"Baada ya mechi ya Simba Day, tulipumzika siku moja, Ijumaa tulianza maandalizi kwa ajili ya mchezo dhidi ya Yanga. Ni mechi ya kutengeneza heshima, kwa sasa tunafanya uchambuzi, mikutano binafsi na ya pamoja ili kuweka mambo sawa," alisema.
Alisema baada ya mchezo huo akili na nguvu zao watazielekeza kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Baada ya hapo tutaelekeza nguvu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, tunaamini umati tuliouona Simba Day tutauona tena tukicheza mechi yetu ya marudiano dhidi ya wapinzani wetu," alisema.
Simba itacheza mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United Jumamosi ijayo, ugenini, kabla ya mechi ya marudiano, Septemba 28, mwaka huu.
Wakati huo huo, uongozi wa klabu ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Crescentius Magori na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu umekutana na benchi la ufundi na wachezaji kuwaeleza mambo mbalimbali kuelekea msimu mpya wa 2025/26.
Kama vile haitoshi, Rais wa Heshima na Mwekezaji, Mohamed Dewji, naye pia alikutana na benchi la ufundi na wachezaji kuzungumzia malengo ya klabu kuelekea msimu mpya wa mashindano.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED