Wachezaji Simba watoa ahadi nzito

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:57 PM Aug 02 2024
Mohamed Hussein 'Tshabalala', na Shomari Kapombe.
Picha: Mtandao
Mohamed Hussein 'Tshabalala', na Shomari Kapombe.

BAADA ya kikosi cha Simba kuwasili juzi kutoka nchini Misri kilipokuwa kwenye kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano, wachezaji wamewashukuru wanachama na mashabiki kwa kumaliza mapema kukata tiketi za kilele cha tamasha la Simba Day kesho, huku wakiahidi kuwalipa kwa kandanda safi la uhakika na ushindi si katika mechi hiyo dhidi ya APR ya Rwanda, bali msimu mzima wa mashindano.

Nahodha wa timu hiyo, Mohamed Hussein 'Tshabalala', amesema kitendo cha wanachama na mashabiki kumaliza tiketi 60,000 za tamasha hilo litakalofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kimewapa nguvu wao kama wachezaji na kimewafanya wawe na kazi ya kufanya ili kuwaburudisha na kuwafurashisha kwa soka safi pamoja na ushindi uwanjani.

"Kwa ujumla sisi kama wachezaji imetupa morali sana kuwa mashabiki wetu wanatufuatilia, wanatupenda na wapo karibu na sisi kwa vipindi vyote. Kwa ujumla tumefanya maandalizi mazuri sana, tunawaita wanachama na mashabiki wa Simba wenye tiketi zao mkononi waje waione timu yao, waangalie ni kitu gani ambacho tumekifanya nchini Misri, naamini msimu huu utakuwa ni bora sana kwetu," alisema nahodha huyo.

Tshabalala hakutaka kabisa kuuzungumzia mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, akisema kwa sasa akili yao watu wote, viongozi, makocha na wachezaji ni katika tamasha la Simba Day tu na si vinginevyo.

"Kwanza tuna mchezo Jumamosi wa Simba Day dhidi ya APR ya Rwanda, mechi ya tarehe nane tutaizungumzia baada ya tamasha letu kupita," alisema.

Naye winga wa timu hiyo, ambaye alisajiliwa kipindi cha dirisha dogo msimu uliopita akitokea Prisons, Edwin Balua, alisema kambi yao ilikuwa nzuri na kila kitu kimekwenda kama kilivyopangwa, hivyo kitendo cha mashabiki kumaliza tiketi zote kinaonesha kuwa wana imani nao.

"Maandalizi yalienda vizuri sana, vitu vizuri tumevifanya inavyotakiwa, Wanasimba wajiandae kupata vitu vizuri," alisema mchezaji huyo.

Naye meneja aliyerejea tena kwenye timu hiyo, Patrick Rweyemamu, alisema wamemaliza awamu kubwa ya maandalizi kilichobaki ni mambo madogo tu, lakini akiwa na imani kubwa ya kufanya vyema msimu huu.

"Tumemaliza awamu yetu kubwa, kwa maana ya msimu mpya kuelekea 2024/25, tumejiandaa vizuri na tuna imani tutafanya vizuri kwa msimu huu,"alisema.

Wakati huo huo, wasanii maarufu kutoka Arusha, Wadudu, wametoa wimbo watakaoutumia kwenye tamasha la Simba Day, uitwao 'Ubaya Ubwela', neno ambalo ndiyo kauli mbiu ya klabu hiyo kwa msimu huu.

Wadudu ni moja kati ya wasanii waliopewa fursa ya kutumbuiza kesho, kwenye tamasha la 16 la klabu hiyo tangu lianzishwe.

Kabla ya mchezo husika kutakuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii wengi mashuhuri nchini, kabla ya utambulisho wa wachezaji wote wa zamani na wapya, ambao watatumika kwa msimu ujao wa mashindano.

Wachezaji wapya wa Simba wanaotarajiwa kutambulishwa ni Jushua Mutale, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoa, Debora Fernandes Mavambo, Augustine Okajepha, Valentin Nouma na Karaboue Chamou, ambapo wazawa ni, Abdulrazack Hamza, Valentino Mashaka, Omari Omari, Kelvin Kijili na Yusuph Kagoma.

Simba ilifanya tamasha lake la kwanza Agosti 8, mwaka 2009, ambapo ilicheza na SC Villa ya Uganda kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) na kushinda bao 1-0 lililowekwa wavuni na Hirally Echessa na baada ya hapo kila mwaka limekuwa linafanyika hadi leo.