Yanga yakwaaa kisiki Mbeya

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:52 AM Oct 01 2025
news
Picha Mtandao
Wachezaji wa Yanga na Mbeya City wakati wa mechi jana.

BAADA ya kushinda michezo 13 mfululizo, mabingwa watetezi, Yanga wameshindwa kufanya hivyo kwa kulazimishwa suluhu dhidi ya wenyeji Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Sokoine, jijini Mbeya jana.

Mbeya City imekuwa timu ya kwanza msimu huu kuipunguza kasi ikiwa imerejea tena Ligi Kuu ikitokea Ligi ya Championship.

Mara ya mwisho Yanga kutoa sare katika ligi hiyo ilikuwa ni Februari 10, mwaka huu, katika mechi ya msimu uliopita, ilipolamizishwa suluhu dhidi ya JKT Tanzania, baada ya hapo Yanga ilishinda michezo yake yote iliyobaki 12, ukiwamo wa kwanza wa msimu huu dhidi ya Pamba Jiji, iliichapa mabao 3-0.

Yanga pia imeshindwa kufunga bao kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya michezo 13 kupita.
Hata hivyo, iliponea chupuchupu kupoteza mchezo huo katika dakika za majeruhi, pale mchezaji, Mwani Willy, alipokosa bao akiwa yeye na kipa, Djigui Diarra.

Mchezaji huyo alishindwa kuitendea haki krosi ya Daniel Lukandamila na kuwaweka salama Yanga kunusurika kupoteza mechi ya kwanza, tangu Novemba 2, mwaka jana, ilipofungwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC.

Haukuwa mchezo rahisi kama ilivyotarajiwa na wengi hasa Yanga inapokutana dhidi ya Mbeya City mara zote kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, ambapo mara ya mwisho zilipokutana kwenye uwanja huo, Juni 6, mwaka 2023, Ligi Kuu ya 2022/23, zilitoka sare ya mabao 3-3, msimu ambao Mbeya City ilishuka daraja.

Hata hivyo, mechi hiyo kwa kiasi fulani ilikosa ladha kutokana na maeneo kadhaa ya uwanja ambayo hayakuwa rafiki.
Mechi ilianza taratibu, lakini Yanga ndiyo ilianza kufika langoni kwa wenyeji wao dakika ya tatu ya mchezo ilipofanya shambulio lililozaa kona ambayo nusura wajipatia bao kama si kichwa alichopiga, Ibrahim Hamad 'Bacca' kuwababatiza mabeki wa Mbeya City.

Kona hiyo ilipigwa na Mohamed Doumbia ambapo, Bacca aliruka juu na kujitwisha mpira, ukawagonga mabeki wa Mbeya City waliokuwa wamejilundika langoni na kuzua kizaazaa kabla ya kufanikiwa kuufagia kwenye eneo la hatari.

Wenyeji walijibu shambulio dakika ya 10 ya mchezo pale Vitalisy Mayanga alipowatoka mabeki wa Yanga na kuachia shuti kali, lakini lilipaa juu ya lango.

Dakika ya 26, Eliud Ambokile, alipata nafasi nzuri ya kukutana ana kwa ana na kipa, Djigui Diarra, lakini alipoga shuti dhaifu lililoishia mikononi mwa kipa huyo.

Doumbia, alipata pasi safi kutoka kwa Israel Mwenda daiika ya 32, lakini alikuwa na papara na kupiga shuti juu akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya vizuri kuliko alivyofanya kwani hakuwa amekabwa na kubugudhiwa na mchezaji yoyote.

Ambokile kwa mara nyingine tena alikosa utulivu dakika ya 34 na kupiga shuti la mbali lililokwenda nje.

Yanga waliliweka kwenye hatari lango la Mbeya City dakika moja kabla ya mapumziko, pale Pacome Zouzoua alipoambaa na mpira kwenye wingi ya kushoto, akawavuta mabeki kadhaa wa Mbeya City ambao walimfuata kabla ya kupiga krosi ambayo hakukuwa na mchezaji yoyote ulipopita kwenye uso goli ukatolewa kona na Yahaya Mbegu.

Ilikuwa ni nafasi ya wazi mno, krosi hiyo ilipopigwa, kipa Beno Kakolanya naye alikuwa ameshavutika na kumvuata Pacome, mpira uliopigwa ulikuwa unasubiri mtu tu auguse ili utinge wavuni, lakini wachezaji wa Yanga walikuwa mbali na eneo hilo.

Kipindi cha pili, timu zote zilifanya mabadiliko ambayo yaliifanya mechi kuwa ngumu zaidi pande zote.

Kakolanya aliyekuwa kwenye kiwango bora jana, aliruka juu na kuugusa mpira wa krosi uliomfanya Pacome kuingia wmenyewe wavuni badala ya mpora dakika ya 48.

Kipa huyo pia alipangua mpira ya faulo dakika ya 69 uliopigwa kiufundi na Celestin Ecua aliyeingia kuchukua nafasi ya Mohamed Doumbia.

Matokeo hayo yanazifanya timu zote kufikisha pointi nne, Yanga ikicheza mechi mbili, ikishinda moja, Mbeya City ikicheza michezo mitatu, ikishinda moja, sare moja na kupoteza moja pia.

Wakati huo huo, Nasreddine Nabi, anatajwa yuko katika hatua za mwisho za kurejea Tanzania kujiunga na moja ya vigogo wa soka nchini akitokea Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.