Dk. Mwinyi aridhishwa na maendeleo ya biashara Darajani

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 05:33 PM Oct 16 2025
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuridhishwa na hali ya ufanyaji biashara katika eneo la Darajani.

Ameeleza kuwa lengo la Serikali ni kuliimarisha eneo hilo na kuendelea kujenga zaidi ili wafanyabiashara wapate maeneo mazuri ya kufanyia biashara.

Rais Dk Mwinyi ameyasema hayo leo alipokutana na wafanyabiashara na wajasiriamali wa soko la Darajani, akiwa katika mfululizo wa kampeni zake za kuomba kura na kuzungumza na makundi mbalimbali ya wananchi.

Amesema kuwa eneo jingine ni ujenzi wa maegesho katika eneo la Malindi, ili kuondoa utaratibu wa kuegesha magari kiholela, na kueleza kuwa mradi mkubwa wa BIG Z, utakaojenga maduka pembezoni mwa barabara, unakuja na utaongeza haiba ya eneo la mjini.

Akizungumzia barabara ya Malindi hadi Mnazi Mmoja, amesema itatengenezwa na kufanyiwa upanuzi kuwa ya njia nne, pamoja na ujenzi wa maegesho katika eneo la Malindi.

Rais Dk. Mwinyi amesema kuwa katika awamu ijayo, Serikali inakusudia kuongeza fungu la fedha kwa ajili ya utoaji wa mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali, hususan wale waliokopa awali na kurejesha fedha kwa wakati.

Kuhusiana na kodi, amesema Serikali itakaa na Chama Cha Mapinduzi, ambacho ndicho chombo kinachohusika na masuala ya sera, ili kulipatia ufumbuzi suala hilo na kuona uwezekano wa kupunguza kodi. 

Aidha, ameliagiza Shirika la Umeme (ZECO) kuweka transfoma mpya katika eneo la Darajani ili kumaliza tatizo la umeme.

Dk. Mwinyi amewaomba wafanyabiashara na wananchi wamchague kwa kura nyingi ili aweze kurejea madarakani na kutekeleza ahadi anazozitoa hivi sasa, sambamba na kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi kwa ajili ya kudumisha amani na maendeleo.

Wakiwasilisha risala yao, wafanyabiashara wa Darajani Souk wameeleza kunufaika na mageuzi makubwa yaliyofanyika katika eneo la Darajani, ikiwemo mazingira bora ya kufanyia biashara.