Dk. Mwinyi: Hati za mashamba ya karafuu kuimarisha uchumi wa Zanzibar

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 12:15 PM Oct 08 2025
Dk. Mwinyi: Hati za mashamba ya karafuu kuimarisha uchumi wa Zanzibar

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema uamuzi wa Serikali kutoa hati za mashamba ya karafuu kwa wananchi ni sehemu ya mkakati maalum wa kuhakikisha zao hilo linaendelea kuwa nguzo kuu ya uchumi wa Zanzibar.

Amesema Serikali imefanya tathmini ya kina kubaini njia bora ya kuwakabidhi wananchi hati rasmi za umiliki wa mashamba yao, hatua itakayowasaidia wakulima kuwa na uhakika wa umiliki, kuondoa migogoro ya ardhi, na kuongeza uwajibikaji katika utunzaji wa mashamba.

“Kupitia mfumo huu, wakulima wataweza kunufaika zaidi kibiashara, kwani hati hizo zitawawezesha kushiriki kikamilifu katika kutunza mashamba yao sambamba na kuinua thamani ya zao la karafuu,” amesema Dk. Mwinyi.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane itaendelea kuimarisha sekta ya kilimo, hususan kilimo cha karafuu, kwa lengo la kupunguza changamoto kwa wakulima, kuongeza mapato ya taifa, na kulinda zao la kihistoria ambalo limekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar kwa miongo mingi.

“Tumejipanga kuhakikisha kilimo cha mikarafuu kinabaki kuwa chanzo kikuu cha kipato kwa wananchi na uchumi wa taifa. Hati hizi zitakuwa chachu ya maendeleo na uwajibikaji katika sekta hii muhimu,” alisisitiza Rais Mwinyi.