TIMU ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha inayotoa huduma ya elimu ya huduma ndogo za fedha ,imewafikia walimu wa shule za msingi, sekondari na wakuu wa idara za elimu na kuwaelimisha kuhusu masuala ya fedha ikiwamo kujiepusha na mikopo isiyo salama, maarufu kama kausha damu.
Semina hiyo ilifanyika juzi katika ukumbi wa St. Clara, wilayani hapa na zaidi ya walimu 650 walishiriki na kupata fursa ya kujifunza mada nne zikiwamo kujiwekea akiba, mikopo, uwekezaji, na usimamizi wa fedha binafsi.
Mmoja wa washiriki, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mizani, Ephransia Zakayo, alisema kuwa kupitia semina hiyo amejifunza kuwa kabla ya kuchukua mkopo ni lazima kuainisha malengo ya kufanya hivyo lakini pia matumizi ya mkopo na namna ya kupanga kurejesha ili kutokuingia kwenye migogoro.
“Kupitia elimu hii nimejifunza pia umuhimu wa kuwa na vipaumbele katika maisha yetu ya kawaida. Ukiwa na vipaumbele, itakusaidia kutokuwa na tamaa na itasaidia kutokukupeleka kwenye mikopo ambayo hukupanga kuchukua”, alisema Zakayo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kikomakoma, Lukanga Yassin, aliishukuru serikali kwa kuwafikia na kuwapa elimu ambayo imewapa uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwamo kuwa na matumizi sahihi na kuweka akiba wanapopata fedha badala ya kuzitumia zote.
Naye Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Stanley Kibakaya, alisema kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa walimu na wameonyesha nia ya kufanya uwekezaji katika taasisi mbalimbali rasmi.
“Katika makundi mbalimbali tuliyowafikia, wananchi wameahidi kubadilisha mtindo wa maisha ikiwamo kuacha kukopa kwa mazoea lakini pia kuanza utaratibu wa kusoma mikataba kabla ya kusaini ili kupunguza kama sio kumaliza kabisa migogoro ya mikopo” alisema Kibakaya.
Kwa kutambua umuhimu wa elimu ndogo ya fedha kwa wananchi wa Tanzania mwaka 2021, serikali kupitia Wizara ya Fedha ilianzisha rasmi Wiki ya Huduma Ndogo za Fedha ambayo hufanyika kila mwaka, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu ya huduma ndogo za fedha katika ngazi zote za mjini na vijijini.
Kwa sasa, timu ya wataalam hao kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na taasisi zingine za serikali, imemaliza utoaji elimu ya huduma ndogo za fedha kwa wananchi wa mikoa ya Kagera, Singida na Manyara.
Timu hiyo sasa inakwenda katika mikoa ya Rukwa na Kigoma kuwafikia wananchi na kupatiwa elimu ya huduma ndogo za fedha ili kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED