Mavunde aagiza STAMICO kuanza mara moja uchimbaji madini Mlima Wigu

By Christina Haule , Nipashe
Published at 05:53 PM Jul 24 2025
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amelielekeza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuanza mara moja shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo la Mlima Wigu, wilayani Morogoro, ili wananchi waanze kunufaika na kuona thamani ya mradi huo kwa haraka.

Waziri Mavunde ametoa agizo hilo leo wakati wa hafla ya ugawaji wa leseni ya uchimbaji wa madini adimu na muhimu (Rare Earth Elements) kwa Shirika la STAMICO, iliyofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Sesenga, wilayani Morogoro.

Amesema kuwa mradi huo ni fursa muhimu ya maendeleo kwa wakazi wa kijiji cha Sesenga, hasa vijana na wanaume, kwa kuwapatia ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa jamii hiyo.

“Mzunguko wa fedha utakuwa mkubwa, mahitaji yatakuwa mengi, na hivyo kuwa fursa kwa wananchi katika nyanja mbalimbali, ikiwemo ajira kwa kina mama. Hivyo basi, ni muhimu kuongeza juhudi kwenye kilimo ili chakula cha mradi kisitoke nje ya Sesenga,” amesema Waziri Mavunde.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Beatrice Njawa, amesema kuwa sekta ya madini ni ya tatu kwa kuchangia uchumi wa mkoa huo, baada ya kilimo na mifugo, hivyo ni sekta muhimu kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuliwezesha shirika hilo kupata leseni ya uchimbaji wa madini katika Mlima Wigu.

Dk. Mwasse amesema STAMICO imejipanga kuanza kazi mapema kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Sesenga, huku wakianza kwa kuwaajiri rasmi walinzi waliokuwa wakilinda eneo hilo tangu awali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala, ameahidi kuhakikisha ulinzi wa kutosha kwa wawekezaji wote wanaowekeza katika mkoa huo, ili kuweka mazingira mazuri ya kufanikisha maendeleo ya wananchi kupitia sekta ya madini.