Pwani yavunja rekodi mnada wa ufuta: tani 7,000 zauzwa zote

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 01:52 PM Jun 27 2025
 Pwani yavunja rekodi mnada wa ufuta: tani 7,000 zauzwa zote.
Picha: Mpigapicha Wetu
Pwani yavunja rekodi mnada wa ufuta: tani 7,000 zauzwa zote.

Mkoa wa Pwani umevunja rekodi katika msimu wa mnada wa tatu wa zao la ufuta, baada ya kuuza zaidi ya tani elfu saba za zao hilo kwa wanunuzi mbalimbali.

Taarifa hiyo imetolewa na Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Pwani (CORRECU), Hamis Mantawela, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mnada huo uliofanyika Ikwiriri, mkoani Pwani.

“Mkoa wa Pwani umevunja rekodi katika kukusanya zaidi ya tani elfu saba za ufuta na kuuza yote kwa wanunuzi,” alisema Mantawela.

Ameeleza kuwa katika wilaya za Kibaha, Chalinze, Bagamoyo na Kisarawe, kulikusanywa tani 93 za ufuta ambazo ziliuzwa kwa bei ya Shilingi 2,470 kwa kilo moja.

Katika Wilaya ya Kibiti, zilikusanywa tani 2,656 na kuuza kwa Shilingi 2,656 kwa kilo. Wilaya ya Mkuranga ilikusanya tani 1,696 na kuuza ufuta kwa Shilingi 2,440.25 kwa kilo moja.

Kwa upande wa Wilaya ya Rufiji na Ikwiriri, walikusanya jumla ya tani 2,800 ambapo kilo moja ya ufuta iliuzwa kwa Shilingi 2,540.17.

Akizungumzia malipo ya mnada wa kwanza, Mantawela alisema kuwa yamefanyika kupitia vyama 19 vya ushirika (AMCOS) na wakulima wote wamelipwa. Aidha, malipo ya mnada wa pili tayari yamelipwa na wanunuzi, hivyo wakulima wataanza kupokea fedha zao muda wowote kuanzia sasa.

1

Kuhusu ushuru wa AMCOS, alisema unagawanywa kwa asilimia 50 kwa 50 kwa minada yote miwili.

Aidha, aliwapongeza waendesha maghala kwa uaminifu wao katika kuhifadhi ufuta, jambo ambalo limeepusha malalamiko kutoka kwa wanunuzi kuhusu kupungua kwa mizigo.

Kuhusu upatikanaji wa viroba, alisema kuwa vimezalishwa kwa wingi na hivyo hakutakuwa na changamoto yoyote ya upungufu wa vifaa vya kuhifadhi ufuta.

Naye Mwenyekiti wa CORRECU Mkoa wa Pwani, Mussa Mng’reza, aliwahimiza wakulima kuendelea kupeleka ufuta ulio safi kwenye maghala ili wanunuzi wazidi kujitokeza kwa wingi.

Alimpongeza pia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kutafuta wanunuzi wa zao hilo, pamoja na kuanzisha mfumo wa mnada wa kidigitali.

“Sasa mnada unafanyika kwa njia ya mtandao, hata mtu akiwa mbali anaweza kuingia mtandaoni na kufuatilia mnada moja kwa moja,” alisema.

Akizungumzia malalamiko ya baadhi ya wakulima kuhusu bei ya ununuzi kuwa ya chini, alisema kuwa ni kawaida kwa bei kubadilika kila msimu na si lazima bei ya mwaka uliopita ifanane na ya mwaka huu.

“Kwenye biashara mabadiliko ni jambo la kawaida, haiwezekani bei ibaki ile ile kila mwaka,” alisisitiza.

Aliwahimiza wakulima waendelee kupeleka ufuta bora ili kuvutia wanunuzi zaidi.

Mwisho, alizipongeza AMCOS zinazobandika taarifa ukutani kuhusu bei za ufuta na kilo zilizouzwa, hatua inayoongeza uwazi na uaminifu kwa wakulima.

2