RUNALI yakabidhi televisheni ya kisasa Shule ya Sekondari Kikulyungu

By Gideon Mwakanosya , Nipashe
Published at 10:58 AM Sep 29 2025
kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Chama Kikuu Cha Ushirika Cha Wilaya za Ruangwa Nachingwea na Liwale ( RUNALI ) akikabidhi Luninga kwa  Walimu wa Shule ya Sekondari yavKikulyungu  iliopo Liwale ambayo ni kuwasaidia kufundishia wanafunzi kwa  vitendo....
Picha na Gideon Mwakanosya
kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Chama Kikuu Cha Ushirika Cha Wilaya za Ruangwa Nachingwea na Liwale ( RUNALI ) akikabidhi Luninga kwa Walimu wa Shule ya Sekondari yavKikulyungu iliopo Liwale ambayo ni kuwasaidia kufundishia wanafunzi kwa vitendo....

Chama Kikuu cha Ushirika cha RUNALI kimekabidhi televisheni ya kisasa yenye ukubwa wa inchi 50 kwa Shule ya Sekondari Kikulyungu, wilayani Liwale, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Mwenyekiti wa RUNALI, Odas Mpungu, alisema lengo la msaada huo ni kuwawezesha walimu kutumia mbinu za kisasa zaidi za ufundishaji kwa kutumia picha mnato na picha mjongeo kufundisha masomo mbalimbali.

“RUNALI ni chama cha ushirika kinacholenga kuwatumikia wanachama na jamii kwa ujumla. Tunapopata fursa ya kuchangia maendeleo ya elimu au sekta nyingine za kijamii, tunafanya hivyo kwa moyo wa dhati,” alisema Mpungu.

Aliongeza kuwa chama hicho kimekuwa mstari wa mbele kurudisha sehemu ya mapato yanayotokana na mauzo ya mazao ya wakulima kutoka wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale—ambazo ndizo zinazounda RUNALI—ili kusaidia miradi ya maendeleo kwa wananchi.

Kwa upande wake, mwalimu wa shule hiyo, Mohamed Hassan, aliishukuru RUNALI kwa msaada huo, akibainisha kuwa televisheni hiyo itasaidia kuongeza uelewa na ubunifu wa wanafunzi kupitia mafunzo ya kielelezo na video.

“Tunawashukuru sana RUNALI kwa kutambua umuhimu wa elimu. Vifaa hivi vitasaidia kuongeza hamasa ya kujifunza miongoni mwa wanafunzi wetu,” alisema mwalimu Hassan.

Msaada huo ni sehemu ya mikakati ya RUNALI kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua kiwango cha elimu nchini, hususan katika maeneo ya vijijini.