WAKUU wa Wilaya ya Ubungo na Kigamboni jijini Dar es Salaam wamekabidhiwa magari mapya mawili yenye thamani ya Sh milioni 252 kila moja, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhite, amesema magari hayo yamenunuliwa kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 wametekeleza ili kurahisisha shughuli za kuwatumikia wananchi.
“Lengo letu ni kuhakikisha viongozi hawatumii magari chakavu tena. Magari haya siyo anasa, ni chombo cha kazi na yatasaidia kutatua matatizo ya wananchi kwa ufanisi,” amesema Mhite.
Akikabidhi magari hayo katika Ofisi za Wilaya ya Kinondoni, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka viongozi hao kuyatunza magari hayo ili kuwajibika ipasavyo na kuongeza mshikamano kati ya serikali na wananchi.
Katika hatua nyingine, RC Chalamila aliwapongeza wachezaji wa timu ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushiriki michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) lililofanyika jijini Mwanza, ambapo timu ya mkoa walitinga fainali ya mchezo wa drafti na kushika nafasi ya pili kitaifa.
“Michezo ni zaidi ya burudani. Ikitumika vizuri ni biashara ni ajira na njia ya kukuza vipaji. Kabla mwaka huu haujaisha, nataka kila wilaya kuunda timu ya mpira wa miguu na pia kuanzisha viwanja vya ngumi ili vijana wetu wapate fursa ya kuonyesha uwezo wao,” amesema Chalamila.
Ameongeza kuwa Dar es Salaam, ikiwa na mapato ya zaidi ya Sh bilioni 300, haina budi kutumia rasilimali zake kukuza michezo na kuinua vipaji vya vijana, huku viongozi wa michezo wakihimizwa kushirikiana na watendaji wa serikali kufanikisha malengo hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED