Marais watano Afrika watinga WhiteHouse

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:48 PM Jul 10 2025
news
Picha Mtandao
Marais waliokaribishwa Whitehouse kwa mkutano na Rais Trump.

RAIS wa Marekani Donald Trump amewakaribisha kwa mazungumzo katika Ikulu ya WhiteHouse viongozi wakuu wa nchi tano za Afrika Magharibi ikiwemo kutoka Liberia, Senegal, Gabon, Mauritania na Guinea Bissau.

Imeelezwa kuwa kwenye kikao hicho masuala kadhaa yamegusiwa ikiwemo ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi, usalama, miundombinu na demokrasia. 

Kwa mujibu wa Ikulu ya White House, mazungumzo hayo kati ya Rais Trump na marais hao kutoka nchi tano za Afrika Magharibi na zenye utajiri wa madini yalilenga kwanza kukabiliana na ushawishi wa Urusi na China barani Afrika lakini pia kujadiliana kuhusu masuala ya usalama, biashara na uwekezaji.

Kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo, Trump ameelezea dhumuni la mialiko hiyo akiwaeleza waandishi wa habari kuwa amewapokea marais kutoka nchi zenye ardhi yenye thamani, madini, mafuta na watu wema.

Pia amesema kuna fursa kubwa za kiuchumi barani Afrika na kwamba analenga kuzidishaushiriki wa Marekani katika bara hilo.

Walipopewa nafasi ya kuzungumza viongozi hao wa Afrika ikiwa ni pamoja na rais wa Mauritania Mohamed El Ghazouani, Bassirou Faye wa Senegal, rais wa Gabon, Brice Nguema, na Umaro Embalo wa Guinea Bissau walimwagia sifa rais Trump huku kila mmoja akinadi kuwa nchi yake inazo rasilimali adimu.

Hata hivyo, Rais wa Liberia Joseph Boakai amesisitiza kuwa nchi yake ingependa kushirikiana na Marekani hasa katika masuala ya amani na usalama. Rais Boakai alipomaliza kuzungumza, Trump alionekana kushangazwa na lafudhi yake nzuri ya kiingereza huku akimuuliza ni wapi alipojifunzia.

Mbali na mazungumzo hayo ya ushiriki wa kibiashara kati ya Marekani na mataifa hayo ya Afriaka, Gazeti la Wall Street limeripoti kuwa Washington ilijaribu pia kuwashawishi marais hao kuwapokea watu wanaofurushwa nchini Marekani.

Mkutano huo pia umekuja katika wakati ambapo rais Trump amefuta msaada kwa mataifa mengi  ya Afrika, hatua ambayo imeanza kusababisha athari kwenye bara hilo.