RAIS wa Malawi anaemaliza muda wake Lazarus Chakwera amekubali kushindwa, na kuliambia taifa hilo kuwa anafanya hivyo kwa kuheshimu nia yao ya kutaka mabadiliko ya serikali.
Rais Chakwera ameyasema hayo leo akihutubia taifa kabla ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa leo mchana.
Matokeo ya awali yanaonesha mpinzani wake, Rais wa zamani Peter Mutharika ameongoza vyema, akijizolea karibu asilimia 66 ya kura zilizohesabiwa kufikia jana.
Katika hotuba yake, Chakwera amesema ametambua matokeo ya kura za awali, jambo ambalo lilionyesha mpinzani wake Peter Mutharika alikuwa ameongoza kwa kiasi kikubwa.
"Ninajua kwamba kwa wengi wenu mliopiga kura, matokeo haya ni taswira ya nia yenu ya pamoja ya kuwa na mabadiliko ya serikali na hivyo ni sawa kukubali kushindwa kutokana na kuheshimu matakwa yenu kama raia," aliwaambia Wamalawi.
Chakwera amesema amempigia simu Mutharika kumpongeza kwa ushindi wake wa kihistoria.
Amethibitisha kuwa alifika mahakamani jana kujaribu kuzuia matokeo yasitangazwe lakini akasema anakubali uamuzi wa mahakama kwamba Tume ya Uchaguzi lazima iendelee na kutangaza matokeo.
Chakwera pia amesema: "Wamalawi, kama mko upande wa kushindwa au kushinda, tafadhali muwe na amani."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED