Urusi na Ukraine zitafanya mazungumzo mapya ya amani kesho Jumatano baada ya duru mbili za mazungumzo huko Istanbul ambazo hazijapiga hatua katika kumaliza vita vyao, ametangaza Rais Volodymyr Zelensky.
"Leo, nilijadili na [mkuu wa Baraza la Usalama la Ukrainian] Rustem Umerov maandalizi ya mkutano mwingine nchini Uturuki na upande wa Urusi. Umerov amenieleza kwamba mkutano huo umepangwa kufanyika Jumatano," Zelensky alisema Jumatatu katika hotuba yake ya kila siku.
Hata hivyo, chanzo kisichojulikana kimeliambia shirika la habari la serikali ya Urusi, TASS kwamba mazungumzo hayo yatafanyika Alhamisi.
Ikulu ya Kremlin mapema Jumatatu ilionekana kuthibitisha kuwa kuna duru nyingine ya mazungumzo itafanyika, na kuongeza kuwa itaarifu umma tarehe maalum itapochaguliwa.
Zelensky alitangaza Jumamosi kwamba yuko tayari kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin ana kwa ana.
Urusi na Ukraine zimefanya duru mbili za mazungumzo ya amani ya moja kwa moja mwaka huu, ya kwanza Mei 16 na ya pili Juni 2.
Duru zote mbili zilifanyika Istanbul.
Chanzo: BBC Swahili
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED