Rais Samia kuzindua Bandari Kavu Kwala

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:50 PM Jul 22 2025
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.

Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa kufanyika Julai 31, 2025 katika eneo la Kwala, Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 22, 2025 mjini Kibaha, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema Rais Samia atazindua Bandari Kavu ya Kwala, safari ya treni ya mizigo kwa njia ya Reli ya Kisasa (SGR), mapokezi ya mabehewa ya reli ya zamani (MGR) pamoja na Kongani ya Viwanda ya Kwala (Kwala Industrial Park).

Kunenge amesema tukio hilo linaonesha mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwekeza kwenye miundombinu ya usafirishaji, viwanda na bandari kwa lengo la kuongeza tija, ufanisi na kuimarisha uchumi wa taifa.

“Mhe. Rais atafanya uzinduzi rasmi wa safari za treni ya mizigo ya mwendokasi (SGR) ambapo tukio hilo litafanyika katika Kituo Kikuu cha kuunganishia mabehewa ya mizigo na karakana ya treni (Marshalling Yard), kilichopo Kwala,” amesema Kunenge.

Kuhusu Bandari Kavu ya Kwala, Kunenge amesema mradi huo ni wa kimkakati kwa sababu utapunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya asilimia 30. Amebainisha kuwa bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia wastani wa makasha 823 kwa siku, sawa na makasha 300,000 kwa mwaka.

Aidha, Rais Samia anatarajiwa kupokea mabehewa 160 ya mizigo, yakiwemo mabehewa 100 mapya yaliyotolewa na Serikali kwa ajili ya MGR, mabehewa 20 yaliyokarabatiwa, na mabehewa 40 kutoka Shirika la Chakula Duniani (WFP).

Katika uzinduzi wa Kongani ya Viwanda ya Kwala—ambayo inatajwa kuwa kubwa zaidi Afrika Mashariki na inatarajiwa kuwa na zaidi ya viwanda 250—Rais atazindua viwanda saba vilivyokamilika na kuanza kazi, pamoja na viwanda vitano vilivyoko katika hatua mbalimbali za ujenzi.

“Hafla hii muhimu itahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, ikiwa ni ishara ya nafasi ya Tanzania katika maendeleo ya uchumi wa kikanda,” amesema Kunenge.

Ameongeza kuwa eneo la Kwala sasa linachukua sura mpya kama kitovu cha biashara na usafirishaji wa kimataifa (International Logistics Hub), hatua inayotarajiwa kuongeza mapato ya Serikali, kukuza usafiri wa reli, kupunguza uharibifu wa barabara, kutunza mazingira na kuimarisha ushindani wa kikanda.

Nchi jirani zitakazonufaika na uwekezaji huu mkubwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zambia, Rwanda, Burundi, Malawi, Zimbabwe, Uganda na Sudan Kusini.