Watu watatu, akiwemo aliyekuwa anagombea nafasi ya udiwani katika Kata ya Solwa, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Awadh Mbaraka, wamefariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea Julai 19, 2025 asubuhi, katika Barabara ya Ibadakuli.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambayo ilihusisha bajaji aliyokuwa akisafiria Mbaraka, kugongana uso kwa uso na basi la Kampuni ya Frester lililokuwa likiendeshwa na dereva Issa Nicodemas.
Kwa mujibu wa Kamanda Magomi, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi la Frester ambaye alijaribu kulipita gari dogo la abiria huku gari jingine likiwa limeharibika barabarani. Katika harakati hizo, alijikuta akiingia upande wa bajaji na kugongana nayo uso kwa uso.
“Diwani huyo mstaafu alijeruhiwa vibaya kichwani na kuvuja damu nyingi, na alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini,” amesema Magomi.
Aidha, abiria wawili waliokuwa ndani ya bajaji hiyo pia walipoteza maisha katika ajali hiyo, ingawa majina yao hayajatajwa rasmi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Edward Ngelela, amesema kifo cha kada wao huyo kimelikumba chama kwa majonzi makubwa, hasa ikizingatiwa kuwa Mbaraka alikuwa ametangaza nia ya kugombea tena nafasi hiyo ya udiwani.
“Tumempoteza mtu muhimu sana katika safu ya uongozi na huduma kwa wananchi. Alikuwa ni mtumishi aliyejitoa kwa ajili ya maendeleo ya Kata ya Solwa,” amesema Ngelela.
Kupitia ujumbe wa rambirambi uliochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum, aliwataka wananchi na familia ya marehemu kuendelea kuenzi mema ya marehemu huyo aliyoyafanya wakati wa uhai wake.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Ndugu Awadh. Tumempoteza mtu muhimu sana aliyekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo na kutetea maslahi ya wananchi,”
Mazishi ya marehemu Awadh Mbaraka yalifanyika Julai 21 katika Kijiji cha Solwa, yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, CCM, ndugu, jamaa na wakazi wa eneo hilo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED